پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Usikatae Kusema Na Usinune

Usikatae Kusema Na Usinune

Ni kawaida ya wanawake wengine kwamba, wanapo tibuliwa na waume zao, hununa, hukataa kusema, hukataa kushughulikia kazi za nyumbani, hawataki kula, huwapiga watoto, au hulalamika. Wanaamini kwamba kuacha kusema au kuanzisha ugomvi ndizo njia nzuri sana kulipiza kisasi kwa waume zao. Msimamo huu si tu unashindwa kumwadhibu mwanaume, lakini unaweza kusababisha naye kulipiza kisasi. Maisha huanza kuwa magumu kwani hugeuka kuwa na mfululizo wa ugomvi. Mwanamke hupiga kite, halafu mwanamume naye hufanya hivyo. Mwanamke hukataa kusema na mwanamume hulipa kisasi. Mwanamke hufanya kitu kingine, na mwanamume hufanya hivyo hivyo hadi wanachoka na kupitia upatanishi wa ndugu au marafiki, huelewana. Lakini hii si mara ya kwanza wao kugombana. Watagombana tena na tena na patakuwepo na siku chache za machungu.

Kwa hiyo, kuishi maisha yenye ugomvi wa familia litakuwa si jambo la kufurahisha kwa ama wazazi au watoto. Vijana wengi waliozikimbia familia zao wanatoka kwenye familia za aina hii ambao baadaye huingia kwenye uhalifu na uovu.

Kijana ambaye alikamatwa kwa tuhuma ya wizi, aliwalaumu wazazi wake kwa uhalifu wake na alisema: “Wazazi wangu walikuwa wakibishana kila siku na baadaye kwenda kwa ndugu zao na mimi nilikwenda kuzurura mitaani. Halafu nikadanganywa na vijana wengine na hatimaye nikafanya uhalifu wa wizi.”

Msichana mwenye umri wa miaka kumi aliwaambia wafanya kazi wa usitawi wa jamii: “Sina uhakika lakini nakumbuka kwamba siku moja wakati wa usiku wazazi wangu walibishana kuhusu kitu fulani. Kesho yake, mama yangu aliondoka na baada ya siku chache, baba alinipeleka kwa shangazi yangu. Baada ya kipindi fulani mwanamke mkongwe alinichukua kutoka kwa shangazi na akanileta Tehran. Ni miaka michache iliyopita hadi sasa, ambapo nimekuwa ninaishi naye na niliteseka sana hivyo kwamba sitaki kurudi kwake.”

Mwalimu wa msichana huyo alisema; Huyu msichana ni mmojawapo wa wanafunzi wangu. Hana maendeleo mazuri katika masomo yake na inaonesha kama vile anaumizwa na jambo fulani. Wakati wote anafikiri. Amekuwa hata anakaa kwenye ua wa shule na kuonekana hayuko tayari kurudi nyumbani. Siku mbili zilizopita nilimuuliza kwa nini hataki kwenda nyumbani? Akajibu kwamba alikuwa anaishi na mwanamke mzee ambaye alikuwa mbaya sana kwake na kwamba hakutaka kurudi nyumbani kwa bi kizee huyo. Nilimuliza kuhusu wazazi wake na akasema walitengana.”

Bibi mpendwa! Lazima ukumbuke kwamba kama mume wako anakuwa mkali sana kwako na hataki kusema na wewe, halafu anaweza hata kuchukua hatua kali zaidi kama vile kukupiga.

Inawezekana labda utaondoka kwenda kwa wazazi wako kwa sababu ya ukali wake. Kitakachofuatia ni kwamba wazazi wako wanaweza wakaingilia kati, na ugomvi wako na mume wako utazidi kupanuka. Hatimaye labda unaweza kuachika ambapo wewe utapata hasara zaidi kuliko mume wako. Inawezekana ukaendelea kuishi peke yako katika uhai wako wote. Kwa hakika utajuta kutalikiwa.

Mwanamke alisema: “Kipindi fulani kilichopita niliolewa. Sikuwa na uelewa mzuri kuhusu kumtunza mume wangu na yeye hakuwa na ujuzi wa kutosha kunitunza mimi. Ilikuwa tabia yetu kugombana kila siku. Wiki moja nilikiwa sisemi naye na wiki moja baadaye alikuwa hataki kusema na mimi.

Mnamo siku za Ijumaa tu, tulikuwa tunaelewana, kupitia kwa upatanishi wa marafiki na ndugu. Pole pole mume wangu alikasirishwa na mimi na alifikiria kunitaliki na kuoa mke mwingine. Kwa kuwa nilikuwa na umri mdogo, sikuwa tayari kubadilika na sikukataa kutalikiwa. Tuliachana na mimi nilipanga nyumba ya kwangu mwenyewe. Baada ya muda mfupi nikatambua hatari. Watu wengi niliokutana nao lengo lao kubwa lilikuwa kunidanganya. Niliamua kupatana na mtaliki wangu na nilikwenda nyumbani kwake. Huko nilimkuta mwanamke ambaye alijijulisha kwangu kama mke wa mtalaka wangu. Nililia njia yote nilipokuwa narudi kwangu. Nilijuta kwa nini nilikubali kuachika, lakini nilichelewa sana.”

Mwanamke mwenye miaka ishirini na mbili, alimpeleka mtoto wake kwa wazazi wake, baada ya kuachika, alijaribu kujiua muda wa usiku, siku ya harusi ya dada yake.

Mama mpendwa! Lazima kwa kweli uepuke kumnunia na kukataa kusema na mumeo. Kama mumeo amekutibua uwe mvumilivu. Ukisha tulia na kuwa makini, ongea naye kwa upole kuhusu kukasirika kwako. Mathalan, unaweza kumwambia: “Ulinifedhehesha jana, au ulikataa kusikiliza matakwa yangu… Hivi ni haki kwamba unaweza kunitendea hivyo?”

Njia kama hivyo, si tu inakupumzisha kwenye hisia zako, bali pia itampa onyo. Kwa hiyo, mumeo atajaribu kurekebisha tabia yake na atakuheshimu kwa tabia yako njema. Matokeo yake atapitia upya tabia yake, na atajaribu kuwa na nidhamu.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wakati Waislamu wawili wakikataa kusemeshana na wasipopatana kwa muda wa siku tatu, wote wawili watakuwa wamevua joho la Uislamu, na hapatakuwepo na urafiki wowote baina yao. Halafu yeyote miongoni mwao ambaye ataanza kupatana na mwenzake, siku ya ufufuo ataishia Peponi (haraka kuliko mwenzake.)”