Utangulizi

Hamu kubwa sana ya vijana wote wanaume na wanawake ambao hufikia umri wa balekhe ni kuoa au kuolewa. Kwa kuanzisha maisha ya pamoja ya ndoa, wangepata kujitegemea zaidi na pia kupata mwenza mwema na wa kuaminika. Wanaangalia maisha ya ndoa kama mwanzo wa ustawi wa maisha yao.

Mwanaume ameumbwa kwa ajili ya mwanamke halikadhalika mwanamke ameumbwa kwa ajili ya mwanaume. Kila mmojawao anao mvuto kwa mwenzake kama sumaku. Ndoa na kuanzisha maisha ya pamoja ni hamu ya kawaida ya mwanadamu na ya kukubaliana na silika zao.

Ndoa inafikiriwa kuwa mojawapo ya neema kubwa sana kutoka kwa Mungu. Kwa kweli ni wapi kwingineko ambako mtu angeweza kupata hifadhi bora zaidi kwa ajili ya ujana kuliko kitengo cha familia yenye kuaminika?

Ni hamu ya kupata familia ambayo humlinda kijana asifuatilie njozi zisizo na mantiki na duku duku la ndani.

Muungano wa ndoa huwawezesha wahusika kupata mwenza mwema na mwaminifu ambaye ataweza kuwa tayari kushirikiana katika wakati mgumu na wa matatizo.

Mkataba mtakatifu wa ndoa ni kamba ya Mungu inayoziunganisha nyoyo, huzibembeleza zinapokuwa zimefadhaika na kuzielekeza njozi zisizo na mantiki kwenye lengo lililo bora. Familia ni kituo cha mapenzi, wema na urafiki ambapo ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa starehe.

Mwenyezi Mungu Mweza wa yote ameitaja neema hii kwenye Qur’an Tukufu:

(وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ (21

“Na katika Ishara zake ni kuwa Amekuumbieni wenza kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.” ( Quran 30:21)

Mtume (s.a.w) wa Uislamu alisema: “Mwanaume ambaye hakuoa hata kama ni tajiri kwa hakika ni masikini na mhitaji; na hivyo hivyo kwa mwanamke.”

Imam Sadiq (a.s) alimuuliza mtu, “Je! Umeoa?” Mtu huyo akajibu, “Hapana” Imam aksema: “Nisingependa kuishi bila kuoa hata kwa usiku moja tu, hata kama ningekuwa nina miliki dunia yote.”

Mtukufu Mtume (s.a.w) akasema: “Hakuna taasisi katika Uislamu iliyobuniwa na Mwenyezi Mungu ambayo anaipendelea na kuipenda zaidi kuliko ndoa.”

Pamoja na kwamba Mwenyezi Mungu Mwenye huruma amewajaalia wanadamu neema yenye thamani kubwa kama hii, wao hawaifurahii, na wakati mwingine kwa sababu ya ujinga na ubinafsi, huugeuza muungano huu wa upendo na ulio barikiwa kuwa jela yenye giza au hata jahanamu iwakayo moto!

Hii ni kwa sababu ya ujinga wa mtu mwenyewe kwamba, jamaa wa familia wanalazimika kuishi kwenye jela hili yenye giza au kwamba mkataba huu wa ndoa takatifu unavunjiliwa mbali.

Kama wanandoa wanafahamu wajibu wao na kutenda kufuatana na maelekezo yake, basi nyumba itakuwa mahali pa urafiki na kufanana na Pepo.

Lakini, kama zipo tofauti za kifamilia na mabishano, nyumba ya familia, kwa kweli itageuka kuwa jela. Tofauti za kifamilia huletwa na sababu mbali mbali, kama vile hali ya kiuchumi, historia ya familia ya mwanaume na mwanamke, mazingira ya maisha, uingiliaji usio na sababu wa baba, mama na ndugu wa pande zote mbili, na sababu zingine nyingi.

Lakini, kwa mujibu wa mwandishi, jambo muhimu zaidi ni ujinga wa mume na mke kuhusu wajibu wao na kutojitayarisha vya kutosha kukabiliana na maisha ya ndoa. Kwa jumla, ili kazi itimizwe, utaalamu na matayarisho ni sifa muhimu zinazohitajika. Kama mtu anakosa ujuzi muhimu na matayarisho, basi hawezi kufuzu katika kufanikisha lengo analo litaka. Hivyo, madarasa ya kuwafundisha na kuwaelimisha watu kwa ajili ya majukumu mbali mbali huanzishwa.

Utaalamu, utayarishaji na ujuzi ni sifa zinazohitajiwa pia katika ndoa. Kijana wa kiume lazima awe na taarifa za kutosha kuhusu kanuni za maadili ya mke wake na matamanio yake ya moyo. Lazima pia afahamu matatizo ya ndoa na njia za kuyatatua. Asifikirie ndoa kuwa kama kununua mali, kukodisha mfanya kazi wa kike, lakini akubali kwamba ndoa ni mkataba wa urafiki, uaminifu, wema, ushirikiano na muungano katika maisha ya pamoja ya familia.

Kijana mwanamke pia lazima afahamu falsafa ya maisha ya mume wake na matakwa yake. Asifikirie kwamba ndoa ni kama kumwajiri mtumishi kwa lengo la kutimiza mahitaji bila ya mapatano na masharti; lakini kama ahadi ya urafiki wa ushirikiano na muungano katika kufanya jitihada kwa ajili ya kuendesha maisha. Ili kuweza kupata ushirikiano ulio fuzu, ipo haja ya kuelewana, ushirikiano na moyo wa mapenzi.

Ingawa maisha ya baadaye ya vijana wa kiume na wa kike zaidi hutegemea ndoa ambayo inahitaji utambuzi wa umuhimu wa fikra za ndoa na matayarisho ya kuifanya kazi kama hii, kwa bahati mbaya jamii yetu hupuuza umuhimu wa masharti haya.

Zaidi wazazi huzingatia mambo kama mahari, uzuri wa sura na haiba. Hata hivyo, hupuuza kujiweka tayari kwa ajili ya kuanzisha maisha ya ndoa kama sharti muhimu. Wanawaoza watoto wao wa kiume na wa kike bila kuwapa taarifa ya kutosha kuhusu maisha ya familia.

Matokeo yake, vijana wawili na watu wasio na uzoefu huingia kwenye maisha mapya na kukabiliana na matatizo mengi. Kutofautiana, mabishano na kupigana huanza kujitokeza. Hapo sasa wazazi wao ndio huingilia kati kwa lengo la kusaidia kusuluhisha migongano. Lakini kwa kuwa uingiliaji wao huwa wa upendeleo zaidi, migongano hukuzwa na hali huwa mbaya zaidi.

Miaka ya kwanza ya maisha ya familia huwa imejaa matukio na matatizo mengi. Hiki ni kipindi ambapo familia nyingi huvunjika kwa kutalikiana na kutengana.

Baadhi yao huendelea na ndoa zao na kupendelea jela hii ya kujitakia wenyewe kuliko kutalikiana, na familia nyingine hujifunza zaidi kuhusu mwenziwe na hutengeneza kiasi fulani cha maisha ya starehe.

Ingekuwa ubora ulioje kama pangekuwepo na jinsi ya kuwaeleimisha na kuwafahamisha vijana wa kiume na wa kike kuhusu misingi na uanzishwaji wa ndoa katika namna ya madarasa yatakayoitwa “matayarisho ya ndoa” ambayo yangewatayarisha wao kuanzisha familia zao. Ninayo matumaini kwamba ipo siku ambapo utaratibu kama huo utaanzishwa.

Kitabu hiki kimeandikwa katika misingi ya umuhimu huu. Katika kuanzimia masuala ya kitabu hiki, nimetegemea Qur’an Tukufu, hadith za Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na Maimamu maasum (a.s.) pia na takwimu za kawaida na uzoefu wangu mwenyewe.

Ingawa miongozo fulani ya ndoa iliyo bora imeandikwa, siwezi kudai kwamba matatizo yote ya familia yanaweza kutatuliwa kwa kusoma kitabu hiki. Inatumainiwa kwamba kitabu hiki kitaonesha ujuzi na utambuzi ulio bora zaidi kwa wale wanaoyapitia matatizo ya ndoa na familia.

Inategemea sana kwa hao wenye madaraka ambao wataona umuhimu wa jambo hili, kuchukua hatua za maana ili kuweza kuwasaidia wale wanaosumbuliwa na maumivu na mateso ya kuharibika na migongano ya familia (Insha Allah).

Kitabu hiki kimegawanywa katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inahusu wajibu wa wanawake kwa waume zao na sehemu ya pili inazungumzia wajibu wa wanaume kwa wake zao. Lakini wanaume na wanawake wanatakiwa kusoma sehemu zote mbili ili waweze kupata ujuzi mzuri wa jambo hili. Kwa kusoma sehemu moja tu ya kitabu, msomaji anaweza kuhisi ubaguzi kwa kupendelea upande moja na kuchukia upande mwingine; lakini, kusoma sehemu zote mbili, msomaji atakiri kwamba hivyo sivyo.

Ibrahim Amini
Qum, July, 1975.