پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Neno La Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la “Principles Of Marriage & Family Ethics” kilichoandikwa na Mwanachuoni: Ibrahim Amini.
Ni ukweli ulio wazi kwamba katika jamii yetu hatujishughulishi sana na somo hili, kana kwamba Uislamu hausemi chochote kuhusu maudhui hii. Ni jambo la kusikitisha kwamba tunawaozesha watoto wetu bila kuwafundisha kanuni za ndoa na maadili ya familia. Matokeo yake ni kwamba, kwa vijana wetu kukosa somo hili muhimu, kumekuwa na migongano mingi na mizozo isiyokwisha katika maisha yao ya ndoa, na hatimaye ni talaka zisizokifani na za kiholela mno katika jamii yetu.

Katika kitabu hiki mwandishi amefanya jitihada kubwa kufanya utafiti na uchunguzi wa kina wa somo la mfumo wa maadili ya familia na uhusiano wa mume na mke, kwa mtazamo wa Kiislamu. Tumekiona kitafaa sana katika jamii yetu hii ambayo imemomonyoka mno kimaadili kwa kuiga tamaduni za kimagharibi ambazo zimewapotosha wengi katika vijana wetu.

Kwa ajili hii tumeona tukitoe kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ili jamii yetu, hususan vijana wetu wanaotarajia kufunga ndoa na wale ambao tayari wako kwenye ndoa wanufaike na somo hili, ambalo kwa hakika ni muhimu sana. Na hili likuwa ndilo lengo kubwa la Taasisi yetu ya ‘Al-Itrah Foundation’ katika kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru ndugu yetu Salman Shou kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vile vile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitakuwa ni mwanga kwa wasomaji wetu na kuzidisha upeo wao wa elimu katika dini.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S.L.P. 19701
Dar-es-Salaam.
Tanzania.