پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Uwe Safi Na Mrembo Nyumbani Pia

Uwe Safi Na Mrembo Nyumbani Pia

Ni desturi ya wanawake wengi kwamba huvaa nguo zao nzuri na kujipamba sana, wakati wanapokwenda kwenye hafla au mikutanoni. Hata hivyo, wanaporudi nyumbani wanavua hayo mavazi mazuri na kuvaa nguo za zamani na chakavu. Wanawake hawa hawako makini na usafi nyumbani na hawajipambi. Wanapokuwa nyumbani nywele zao zinakuwa timtim, nguo zenye madoa na soksi zilizotoboka.

Kwa kweli hali inatakiwa ibadilishwe kabisa kwa kiasi kikubwa kabisa, kwamba mwanamke anatakiwa ajipambe akiwa nyumbani na awe mchangamfu kwa mume wake ili aweze kuvutia moyo wake na ili asiache ufa wowote ambao unaweza kujazwa na wanawake wengine. Kwa nini mwanamke aoneshe uzuri wake kwa watu wengine? Hivi inastahiki mwanamke kuonesha uzuri wake kwa wanaume wengine na kusababisha matatizo kwa vijana?

Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema: “Mwanamke yeyote anayejipaka manukato na kuondoka nyumbani hawezi kupata neema za Mwenyezi Mungu Mweza wa yote hadi anaporudi nyumbani.”

Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Mwanamke bora zaidi miongoni mwa wanawake ni yule ambaye ni mtiifu kwa mume wake, hujiremba kwa ajili ya mume wake lakini haoneshi urembo wake kwa wageni na mwanamke mbaya kuliko wote miongoni mwa wanawake wenu ni yule anayejipamba wakati mumewe hayupo.”

Bibi mpendwa! kuuteka moyo wa mwanaume hususan kwa muda mrefu si rahisi, Usifikirie hivi kwamba: “Ananipenda, hivyo Sihitaji kuonekana mrembo kwake au kujaribu kushinda moyo wake au kumshawishi.” Lazima udumishe mapenzi yako kwake kila siku. Uhakikishe mume wako atafurahi kuwa na mke safi na mrembo hata kama hawezi kutamka. Kama ukishindwa kuridhisha matamanio ya moyo wake na huvai nguo za kuvutia unapokuwa nyumbani, anaweza akawaona wanawake wazuri wenye kuvutia nje ya nyumba.

Anaweza akakatishwa tamaa na wewe na anaweza kuelekeza mapenzi yake nje ya njia iliyo nyooka. Akiwaona wanawake wazuri anawalinganisha na wewe. Kama wewe ni mchafu, mzembe, na nywele zako ni matimtim, anaweza akadhani kwamba wanawake wengine ni malaika ambao wameteremka kutoka mbinguni. Kwa hiyo jaribu kuonekana unapendeza na kuvutia wakati ukiwa nyumbani na uhakikishe kwamba atavutiwa na wewe kila wakati.

Soma barua ifuatayo iliyoandikwa na mume: “Mtu hawezi kubainisha mke wangu na mtumishi wangu wa ndani ya nyumba. Ninaapa kwa jina la Allah kwamba wakati mwingine hufikiri: natamaani angevaa nyumbani mojawapo ya mavazi haya yalioshonwa kwa ajili ya karamu. Natamani angetupa zile nguo zilizochakaa. Nimemwambia mke wangu mara kadhaa; Mpenzi angalau vaa zile nguo nzuri hapa nyumbani unapokuwa likizo. Akajibu kwa ukali ‘ Sihitaji kwa tofauti ninapokuwa nyumbani, lakini kama siku moja ninaonekana mchafu, mbele ya wafanyakazi wenzangu, nitaona aibu.’ ”

Msomaji anaweza kuamini kwamba wakati mwanamke anaangalia usafi wa nyumba na kupika hawezi kuvaa vizuri na kupendeza.

Hii inawezekana kuwa kweli lakini mama wa nyumba anaweza kuwa na nguo tofauti za kuvaa wakati wa kufanya usafi wa nyumba; na anaweza akabadilisha nguo zake za kufanyia kazi anapokuwa mbele ya mume wake au anapokuwa amerudi nyumbani. Wakati wote unaweza kuchana nywele zako na kujiweka katika hali ya usafi baada ya kufanya usafi wa nyumba.

Imamu Baqir (a.s) alisema: “Ni wajibu wa mwanamke kujipaka manukato na kuvaa nguo nzuri sana, kujipamba kadiri iwezekanavyo, na kukutana na mume wake katika hali hii mchana na usiku.”

Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Wanawake hawatakiwi kuacha kujiremba iwe hata kuvaa kidani tu. Usiwe na mikono isiyo tiwa rangi kidogo, hata kama ni hina kidogo tu. Hata wanawake wazee wasiache kujipamba.”