پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Malalamiko Na Manung’uniko

Hakuna mtu yeyote asiyekuwa na matatizo na manung’uniko kuhusiana na maisha ya kila siku. Kila mtu hupenda kuwa na mtu wa kumhurumia ambaye anaweza kuwa mwandani wake na kumsikiliza matatizo yake. Lakini jambo la kukumbuka ni kwamba “upo wakati na mahali kwa kila jambo.” Mtu lazima aelewe wakati muafaka na mahali pa kulalamikia. Baadhi ya wanawake wajinga na wabinafsi hawatambui kwamba waume zao wanachoka sana na fadhaa baada ya kazi ya siku nzima. Badala ya kungoja kwa muda wa saa moja au mbili ili apumzike na kupata nguvu, huanza kumshambulia kwa mfululizo wa malalamiko. Mathalani mke anaweza kusema:

“uliniacha mimi na watoto hawa maluuni na ukaenda zako. Ahmad amevunja kioo cha mlango wa chumba cha mbele. Watoto wetu wa kike walipigana. Makelele ya watoto wa majirani zetu yananiudhi kweli. Hasan hajifunzi hata kidogo na amepata maksi za chini sana. Nimefanya kazi sana leo najisikia nimechoka. Hakuna hata mtu wa kusikiliza kilio changu!

“Watoto hawa hawanisaidii hata kidogo kwa kazi za hapa ndani. Afadhali nisingezaa watoto kabisa! Unayo habari dada yako alikuwa hapa leo? Sijui tatizo lake nini; alikuwa anafanya mambo kama vile nimemeza urithi wa baba yake.

“Mungu na aninusuru kutoka na mama yako! Amekuwa ananisengenya. Nimechoshwa na wote hao. Pia nimejikata kidole leo kwa kisu na kuumia sana.

“Ingekuwa vema kama nisingekwenda kwenye harusi ya Muhamedi jana. Ungemuona mke wa Rashid! Alivyopendeza, ungeshangaa! Mwenyezi Mungu angenipa na mimi bahati kama hiyo! Wanaume wengine wanawapenda wake zao na huwanunulia vitu vizuri. Hao ndio waoaji wa kweli.

“Rashid alipoingia kila mtu alimpa heshima. Ni kweli kwamba watu hupendelea kuona tu vazi ulilovaa. Anacho nini ambacho mimi sina? Kwa nini ajioneshe mbele yangu? Ndio, anayo bahati kuolewa na mume ambaye anampenda, yeye si kama wewe!

“Siwezi kuvumilia kuendelea kuishi kwenye nyumba iliyolaaniwa, kukutunza wewe na watoto. Kwa hiyo fanya utakalo!”

Msimamo wa namna hi si sahihi. Wanawake wa aina hii hudhani kwamba waume zao huondoka kwenda kwenye pikiniki au burudani kila asubuhi. Wanaume hukutana na mamia ya matatizo kila siku. Bibi mpenzi! Hujui mumeo amepita kwenye mambo gani anapokuwa katika kazi yake. Hujui ni watu fidhuli na wenye karaha kiwango gani mumeo ameshughulika nao siku nzima. Kwa hiyo, anapokuja nyumbani usiwasilishe malalamiko yako yote kwa wakati moja. Usimfanye ajihisi kuwa imekuwa hatia kuwa mwanamume.

Uwe na wastani na umfikirie. Endapo kwa kunung’unika kwako na kumsumbua, kutamuongezea wasi wasi na machungu, basi, ama anaweza akaanza ugomvi au akaondoka hapo nyumbani na kwenda kwenye mgahawa au filamu au hata kutembea tu mitaani.

Kwa hiyo, ewe Bibi mpenzi! Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, acha mazoea haya ya kulalamika hata wakati usio muafaka. Tafuta muda unaofaa na halafu mpe matatizo yako ambayo ni ya kweli, si kwa kulalamika, lakini fanya hivyo, kwa namna ya kushauriana. Kwa njia hii, hutasababisha yeye kuanza kujenga hisia za uadui na mapatano ya familia yanabaki kuwa salama.

Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema:

“Sala za mwanamke anayemchokoza mume wake kwa ulimi wake, hazikubaliwi na Mwenyezi Mungu hata kama akifunga saumu kila siku, anaamka kila siku usiku kufanya ibada, anawaachia huru watumwa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mwanamke mwenye ulimi mbaya ambaye humuumiza mumewe kwa njia hii, ni mtu wa kwanza kuingia Jahanamu!”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) pia alisema: “Wanawake wa Peponi huwaambia wanawake wanaowatukana waume zao kwa njia hii: ‘Mwenyezi Mungu na akuuweni. Msiwe watovu wa adabu kwa waume zenu. Mtu huyu (mume) si kiumbe wako, na wewe hustahiki kuwa naye. Muda mfupi ujao atakuacha na atakuja kwetu.’ ”

Sijui wanawake wa aina hii wanataka kujipatia nini kwa hayo manung’uniko yao. Kama wanataka kusikilizwa na waume zao au kujionesha, basi, hakika wanajipatia kitu kinyume chake kabisa na kumkasirisha. Kama wanakusudia mateso kwa mume, kumsababishia madhara ya kisaikolojia na kumuingiza kwenye mazoea bandia ya kuangamiza, basi wapo kwenye njia potofu.

Bibi mpendwa! Kama unamjali mumeo na familia yako, basi ni lazima uache msimamo huu usio na mantiki. Je, umewahi hata kufikiria kwamba mwenendo wako mbaya unaweza ukasababisha kuvunjika kwa maisha ya familia yako?

“Daktari mmoja alitoa ushahidi mahakamani: ‘Sijapata kumuona mke wangu akifanya mambo kama mke sahihi wa nyumbani wakati wote wa ndoa yetu. Nyumba yetu mara nyingi imekuwa katika machafuko.Wakati wote mke wangu anapiga makelele na kutukana. Nimechoshwa naye.’ Baada ya kumlipa mke wake fedha nyingi tu, akapata talaka. Akasema kwa furaha: ‘Kama angetaka na angeomba utajiri wangu wote na hata shahada yangu ya taaluma ya tiba, ningempa ili niachane naye haraka sana.’ ”