پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Umama (Utunzaji Wa Watoto)

Umama (Utunzaji Wa Watoto)

Mojawapo ya wajibu wa wanawake ni kutunza watoto wao. Hii si kazi rahisi lakini ni nyeti na muhimu. Ni wajibu wenye heshima na thamani kubwa uliowekwa kwa wanawake kwa amri ya muumbo. Yapo mambo machache ambayo yametajwa hapa kuhusu suala hili:

Tunda la Ndoa - licha ya kwamba mwanaume na mwanamke wanaoana kwa sababu chache kama vile kwa sababu ya ushawishi wa kijinsia, mapenzi na kadhalika, kupata mtoto si sababu mojawapo muhimu ya ndoa.

Lakini huwa haipiti muda mrefu kabla ya nia ya kweli ya maumbile ya asili kudhihirika na mapenzi ya kupata mtoto hukua ndani ya nyoyo zao. Kuwepo kwa mtoto ni tunda la mti wa ndoa na matamanio ya asili ya wanaume na wanawake. Ndoa isiyokuwa na mtoto ni sawa na mti usiokuwa na tunda. Mtoto huimarisha mfungamano wa mapenzi baina ya wanandoa. Huwa kama msukumo kwa maisha ya mwanamume kufanya kazi na hutia moyo wazazi kutunza familia yao.

Wakati mwingine ndoa hutokana na matamanio ya kijinsia ya papo kwa papo. Msingi wa aina hiyo si sahihi na haudumu na kila mara huelekea kwenye uharibifu. Kipengele kinachoimarisha msingi huu ni kuwepo kwa mtoto. Matamanio na msukumo wa kijinsia hufifia haraka sana. Kumbukumbu moja tu inayoendelea kuwepo kuhusu matamanio ya kijinsia ingekuwa watoto, ambao kuwepo kwao huchangamsha nyoyo za wazazi.

Imamu Sajjad (a.s) alisema: “Furaha ya mtu ni kupata watoto wachamungu ambao anaweza kupata msaada kutoka kwao.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Mtoto mcha Mungu ni mmea unao nukia harufu tamu kutoka miongoni mwa mimea ya Peponi.”

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Ijumlishe kwenye idadi ya watoto wenu, kwa sababu mimi, Siku ya Hukumu, nitahisi nimeheshimiwa kuhusu ukubwa wa idadi yenu kuzidi umma zingine.”

Ni wajinga kiasi gani wale ambao, wakiwa na udhuru mbali mbali hukataa kupata watoto, na hivyo hupinga kanuni ya uumbaji!

Kumwelimisha mtoto: Wajibat ambazo ni nyeti kuliko zote za mama ni kazi ya kumwelimisha mtoto na kuwaelekeza. Licha ya kwamba wazazi wote wawili wanatakiwa kugawana wajibu huu, uzito mkubwa zaidi upo kwa mama. Hii ni kwa sababu mama anao uwezo wa kumlinda na kumfuatilia mtoto wakati wote. Kama mama, kwa kupitia kwenye utaratibu ulio sahihi hujaribu kulea watoto wao, halafu taifa lote na hata dunia ingepita kwenye mabadiliko ya kimapinduzi.

Hivyo, maendeleo au kutokuendelea kwa jamii ni mambo ambayo yapo mikononi mwa wanawake. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Pepo iko chini ya nyayo za mama.” Watoto wadogo wa leo ndio wanaume na wanawake wa kesho. Masomo yoyote wanayo jifunza sasa, watayafanyia mazoezi katika jamii zijazo. Kama familia zinaendelea, jamii itaendelea kwa sababu jamii itaendelea kwa sababu jamii ni mkusanyiko wa familia nyingi. Dunia ya kesho itaumia kwa sababu ya kuwepo watoto wenye hasira, jeuri, wajinga, woga, wapenda dunia, wabaya, wazembe, wachoyo na katili.

Kinyume chake dunia ya kesho itafaidika kwa sababu ya kuwepo leo watoto ambao ni waaminifu, wenye tabia njema, wema, jasiri, wapenda haki, wa kutegemewa na kadhalika.

Kwa hiyo, kwa ujumla, wazazi na hasa zaidi mama wanao wajibu kwa jamii zao. Wanaweza kuhudumia jamii zao kwa kulea na kukuza watoto wachamungu. Kwa upande mwingine, uzembe katika utekelezaji wa wajibu wao utahojiwa Siku ya Hukumu.

Imamu Sajjad (a.s) alisema: “Haki ya mtoto wako ni kwamba unatakiwa kutambua kwamba anatoka kwako.

Awe mzuri au mbaya anao uhusiano na wewe. Wewe unawajibika kumlea, kumsomesha na kumuonesha njia inayo elekea kwa Mwenyezi Mungu na kumsaidia awe mtiifu.

Unatakiwa kumshughulikia kwa namna ambayo kwamba ukimtendea wema, utakuwa na uhakika wa kupata thawabu na kama ukimfanyia ubaya, uwe na uhakika wa kuadhibiwa.”

Kama mambo yalivyo, si mama wote ambao wanatambua umuhimu wa stadi za kumwelekeza mtoto na ndio sababu wanatakiwa kujifunza na kuzijua stadi hizo.

Si katika eneo la kitabu hiki kuweka maelezo ya kina kuhusu malezi ya mtoto. Kwa bahati nzuri, vipo vitabu vingi ambavyo vimeandikwa na waandishi na wasomi kuhusu somo hili. Wanawake wanaweza kununua vitabu hivi na kwa msaada wa uzoefu wao wenyewe, wanaweza kuwaelimisha watoto wao na hata kuwa mabingwa katika fani ya malezi ya mtoto. Mama mmoja bingwa anaweza kuwasaidia mama wengine katika kazi zao kuhusu watoto wao.

Hapa linatakiwa kutajwa jambo moja. Watu wengi hufanya kosa kuhusu maneno mawili: ‘elimu’ na ‘maelekezo,’ au hudhani yana maana moja. Lakini mtu anatakiwa kujua kwamba kumfundisha mtoto masomo mbali mbali kama vile hadith zinazo faa, mashairi, Qur’ani, Hadith za Mtume

(s.a.w.w) na Maimamu (a.s) si kumwelimisha. Masomo kama haya yanafaa lakini mtoto si tu ajifunze kuhusu watu waaminifu, lakini yeye mwenyewe anatakiwa kuwa mwaminifu.

Hivyo, lazima tutengeneze hali ya mazingira ya maisha ambayo mtoto kwa kawaida atakuwa mtu mwaminifu na mchamungu. Kama mtoto atakuwa mtu mwaminifu na mchamungu. Kama mtoto atakuwa kwenye mazingira ya uaminifu, ukweli, ujasiri, nidhamu, usafi, wema, upendo, uhuru, haki, uvumilivu kutegemewa, utiifu na kujitoa muhanga, basi hujifunza yote hayo. Kwa upande mwingine, mtoto anayepata makuzi akiwa katika mazingira ya uovu, udanganyifu, hasira, chuki, uaminifu na uasi hataepuka kuathiriwa na mambo hayo. Mtoto kama huyu anaweza kujifunza hadith nyingi, lakini hatanufaika nazo.

Wazazi wasio waaminifu kulea na kukuza watoto waaminifu kwa kuwafundisha Qur’ani na Hadith.

Mama na baba waovu kwa kweli humfundisha mtoto wao kuwa muovu. Mtoto huzingatia zaidi matendo ya wazazi wake na si maneno yao.

Kwa hiyo, wale miongoni mwetu ambao wapo makini kulea watoto waaminifu na wema, lazima kwanza warekebishe tabia zao wenyewe. Hii ndio tu njia ya kumwelimisha mtoto anufaike yeye mwenyewe na jamii yake.