پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Kazi Za Wanawake

Kazi Za Wanawake

Ni sahihi kwamba kutafuta na kupata kipato cha familia ni wajibu wa mwanaume na kwamba wanawake hawaruhusiwi na sheria ya Kiislamu kuwajibika kwa kitendo hiki. Hata hivyo, wanawake pia wanatakiwa kufanya kazi. Katika Uislamu kukaa bure ni fedheha na hukemewa.

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anachukia kulala sana na kupumzika sana.”

Imam Sadiq (a.s) pia alisema: “Kulala sana hupoteza na kuharibu maisha ya mtu hapa duniani na Akhera.”

“Hadhrat Zahra (a.s) pia alikuwa akifanya kazi nyumbani”

Mtu yeyote mwenye kuhitaji na asiye hitaji, anatakiwa kuwa na kazi. Asipoteze bure maisha yake kwa kutofanya lolote, lakini anatakiwa kufanya kazi na kutoa mchango wake katika kujenga dunia iliyo bora.

Kama ni muhimu, mtu anatakiwa kutumia kipato chake kwa ajili ya familia yake na yeye mwenyewe, lakini kama kipato hicho hakihitajiki basi atoe msaada kwa wale wanao hitaji. Kukaa bure huchosha na mara nyingi husababisha maradhi ya kiakili na kisaikolojia na pia ufisadi.

Kazi iliyo bora zaidi kwa wanawake walioolewa ni kutunza nyumba. Utunzaji wa nyumba na watoto na kadhalika ni kazi nzuri na rahisi zaidi ambazo zinaweza kufanywa na wanawake.

Mwanamke aliyeolewa mwenye kipaji na bidii kwenye kazi anaweza kuibadili nyumba yake na kuwa mahali pa Pepo kwa watoto na mume wake; na hii ni kazi inayofaa na yenye thamani.

Mtume (s.a.w.w) alisema: “Jihadi ya mwanamke ni hapo ambapo humwangalia na kumtunza mume wake vema.”

Umm-e-Salamah alimuuliza Mtume (s.a.w.w.w): “Ni thawabu kiasi gani zimekadiriwa kwa kazi ya nyumbani kwa mke wa mtu?” Mtume (s.a.w.w) alijibu: “ Mwanamke yeyote ambaye anaipanga nyumba ionekane nadhifu, anachukua kitu fulani kutoka mahali fulani na kukiweka mahali pengine atafurahia neema za Mwenyezi Mungu, na mtu yeyote mwenye mvuto wa neema za Mwenyezi Mungu, hatateswa na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.”

Umm-e-Salamah akasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Wazazi wangu na watolewe muhanga kwa ajili yako, tafadhali taja thawabu zingine kwa ajili ya wanawake.” Mtume (s.a.w.w) alisema: “Mwanamke anapokuwa mja mzito, Mwenyezi Mungu humpa yeye thawabu nyingi kama zile ambazo angepata mtu anayepigana vita vya Jihadi kwa kutumia utajiri wake na uhai wake. Halafu mwanamke anapojifungua mtoto wake, wito humfikia na kusema, ‘dhambi zake zote zimesamehewa; anza maisha mapya tena.’ Kila anapomnyonyesha mtoto wake maziwa yake, Mwenyezi Mungu humpa thawabu sawa na zile anazompa mtu anapomwacha huru mtumwa katika kipindi anacho mnyonyesha.”

Hata hivyo, hata wanapokuwa hawashughuliki na kazi za nyumbani, wanatakiwa kutafuta kitu cha kufanya, wanaweza kusoma vitabu, kufanya utafiti wa kitu chenye manufaa, ili wajiongezee ujuzi na kustadi wao. Wanaweza kuandika makala na hata vitabu. Wanaweza kuwa wachoraji, mafundi wa kupaka rangi, ufundi cherehani na kadhalika. Matokeo yake ni kwamba wanaweza kusaidia familia zao kiuchumi na pia kutoa mchango kwa jamii yao kwa kudhihirisha mafanikio yao kwa umma.

Kufanya kazi huzuia kuendelea kuwepo kwa maradhi ya akili.

Imam Ali (a.s) alisema: “Mwenyezi Mungu humpenda mchamungu ambaye kwa uaminifu anajishughulisha na kazi.”

Wakati ambapo baadhi ya wanawake hufanya kazi nyumbani, wapo wengine ambao hupenda kazi ya nje. Upendeleo huu ama unaweza kuwa kwa sababu ya kiuchumi au zingine. Kwa vyovyote vile, kazi nzuri kuliko zote ni zile za kitamaduni au uuguzi. Shule za vidudu, msingi, sekondari na sehemu zinazofaa kwa wanwake kufundisha na kuongoza wanafunzi wanawake. Mahospitali pia ni sehemu ambazo zinafaa kwa wanawake kutoa huduma ya uuguzi na udaktari.

Kazi kama hizi zinakubalika kwa maumbile ya kike; na pia mara chache sana, inapobidi wao kukutana na wanamume ambao si mahram (wanaume ambao sio ndugu wa karibu na ambao imeharamnishwa kufunga ndoa nao).

Yafuatayo ni mapendekezo kwa wanawake wenye nia au wanaofanya kazi nje ya nyumba zao:

Pata ushauri kutoka kwa mumeo kabla ya kuanza kufanya kazi. Ni haki ya mueo kukabali au kukataa kukupa ruhusa ya kufanya kazi. Kuanza kufanya kazi bila ruhusa ya mumeo inaweza kusababisha madhara kwenye mazingira tulivu ya kupendana katika familia yenu. Wanaume pia wanashauriwa kuwa wagumu kukubali wake zao kufanya kazi nje ya nyumba zao, isipokuwa kazi husika iwe haifai kwa wanamume.

Wanawake lazima wawe waangalifu kuhusu vazi la Hijabu ya kiislamu wanapokuwa nje ya nyumba zao. Lazima waende kazini bila kujipodoa na wavae nguo zisizo na urembo. Lazima waepuke kuchanganyika na wanaume ambao si mahram kwao kadiri iwezekanavyo. Ofisi ni mahali pa kazi si mahali pa kujionesha au mashindano.

Sifa njema na heshima ni sifa zisizoletwa na kivazi chako, lakini husababishwa na matendo yako, na matendo hayo unayafanua vema kiasi gani. Matendo yako yawe kama mwanamke wa kiislamu anaye heshimika. Dumisha tabia ya kujiheshimu mwenyewe, na usiziumize hisia za mume wako; mapambo yako na nguo zako nzuri sana, vaa unapokuwa nyumbani kwa ajili ya mume wako.

Wanawake wanatakiwa kuwa na tahadhari kwamba licha ya wao kufanya kazi nje ya nyumba zao, bado wanategemewa na waume zao na watoto wao kutoa huduma za shughuli, kama utunzaji wa nyumba, kupika, kufua na kadhalika.

Shughuli hizi zinaweza kufanywa kwa ushirikiano wa kifamilia. Kazi ya nje ya nyumba isiwe sababu ya kuitibua familia yote. Wanaume pia wanashauriwa kuwasaidia wake zao kuhusu utunzaji wa nyumba. Waume wasiwategemee wake zao kufanya kazi nje na nyumbani pake yao. Matumaini ya aina hii wala si halali ama haki. Wanaume na wanawake lazima wagawane kazi za nyumbani.

Kama mwanamke, ambaye anafanya kazi nje ya nyumba anaye mtoto, basi anatakiwa amwache mtoto kwenye shule ya chekechea au mtu anayeaminika na mwema. Wala si haki au busara kuwaacha watoto nyumbani bila mtu wa kuwatunza, kwani watoto wengi huwa waoga au kujihisi hawana msaada wanapo kabiliana na hali ya hatari.

Kama mwanamke anahisi kwamba, zaidi ya kazi zilizotajwa hapo juu na wajibu uliotajwa hapo juu, lazima afanye kazi nyingine, basi ni lazima aelewane na mume wake wazi wazi na aanze kufanya kazi hiyo kwa ruhusa yake na ushauri wake. Kama mume atakataa, mke lazima aache mpango huu. Kama mume atakubali mke wake afanye kazi, lazima achague kazi ambayo itamkutanisha na wageni wanaume wachache sana. Hii ni kwa manufaa yake na jamii. Kwa vyovyote vile, anapokuwa nje ya nyumba yake, lazima awe makini kufuata kanuni za vazi la kiislamu la Hijabu na asijipodoe kabisa.