پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Lishe Na Afya

Lishe Na Afya

Wajibu mwingine muhimu wa mwanamke aliye olewa ni kuwapa chakula watoto. Afya nzuri au ugonjwa, uzuri au ubaya, hata tabia njema au mbaya na ujanja wa watoto, vyote hivi vina uhusiano na lishe wanayopewa.

Watoto wana mpangilio tofauti wa kula kulinganisha na watu wazima.

Watoto wanayo mahitaji mbali mbali katika umri tofauti na kwa hiyo mama wanatakiwa kulifikiria jambo hili wanapo wapa chakula watoto wao.

Chakula kizuri sana na chenye kurutubisha sana ni maziwa. Maziwa yana kila kitu kinachohitajiwa kwa ajili ya mwili wenye afya. Hivyo, hakuna chakula kinachomfaa mtoto mchanga isipokuwa maziwa ya mama yake. Kwa kuwa maziwa yana viambato ambavyo vinafaa kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa mtoto mchanga, kwa hiyo hakuna matatizo ya kumlisha mtoto mchanga maziwa ya mama yake. Zaidi ya hayo, mama hahitaji kuchemsha, kuondoa, vijidudu au kuyasafisha kabisa maziwa hayo. Hakuna wasi wasi wa uhalisi wake.

Imamu Ali (a.s) alisema: “Hakuna chakula kizuri zaidi na kingi zaidi kuliko mazia ya mama kwa mtoto mchanga.”

Daktari A.H. Mkuu wa Eastern Maditeranean Region of World Health Organization wa zamani alisema: “Mojawapo ya kipengele muhimu ambacho husababisha mtoto apatwe na maradhi mengi ni kutokupata maziwa ya mama yake ambayo ndio tu bima ya maisha ya mtu.”

Hivyo, mama wanao nyonyesha watoto wao maziwa yao lazima wakumbuke lishe muhimu kwa watoto wao imo kwenye maziwa hayo.

Lakini maziwa yenye lishe bora ni yale tu yanayotokana na lishe bora ya mama, ubora wa maziwa yake yanahusiana na ubora na wingi wa chakula cha mama. Mama akipata chakula bora zaidi ndivyo na maziwa yake yatakavyokuwa. Mama wanao wanyonyesha watoto wao maziwa yao, kutokana na uzembe wao kuhusu lishe bora wanaweza kuharibu afya zao na zile za watoto wao.

Baba wanaolea watoto wachanga pia wanao wajibu wa kuwapa wake zao chakula cha kutosha na kilicho bora. Utapiamlo ni tatizo kubwa kwa watu wengi kuboresha na mtu hatakiwi kudharau jambo hili au vinginevyo awe tayari kulipa, kugharamia tiba ya maradhi yanayosababishwa na hali hii.

Unaweza kupata taarifa ya kutosha kuhusu somo hili kutoka kwa daktari wako wa tiba au vitabu vinavyo husiana nalo. Lakini kama sharti la ujumla mama anaye nyonyesha anatakiwa kula aina zote za vyakula kuanzia nyama, matunda, vyakula vitokanavyo na maziwa… mpaka mboga za majani.

Ukweli ulio muhimu ni kwamba maziwa ya mama huathiri tabia ya mtoto na ndio sababu Imamu Ali (a.s) alisema: “Msichague wanawake wapumbavu kunyonyesha watoto wenu maziwa yao, kwa sababu maziwa hufanya asili ya ubora wao kupenyezwa kwa mtoto.”

Imam Baqi (a.s) alisema: “Chagueni wanawake waungwana kunyonyesha watoto wenu maziwa yao, kwa sababu asili ya ubora wa maziwa unapitishwa kutoka kwa mnyonyaji hadi kwa mtoto.”

Lazima umnyonyeshe mtoto kwa vipindi. Mtoto wako hupata mazoea kutokana na ulinganifu huu na kumsaidia kuwa mvumilivu. Pia humsaidia kuhusu kuboresha mpangilio wa mmeng’enyeo wa chakula na tumbo. Kwa upande mwingine, kama utamnyonyesha mtoto kila anapolia basi, hatajifunza kuwa na nidhamu. Kama mtoto akizoea kupata atakacho kwa njia ya kulia basi ataichukua tabia hii na kuutumia hata atakapokuwa mtu mzima.

Hatakuwa na umuhimu wa kuvumilia atakapo kabiliwa na shida. Ama atatumia nguvu ili afanikishe matamanio yake au atafadhaika akipatwa na matatizo.

Usidhani kwamba kumfundisha mtoto nidhamu ni kazi ngumu. Lazima uwe mvumilivu na utaratibu unaofaa wa kumwelekeza kufuatana na kiwango chako. Wataalam wa lishe ya mtoto wanasema kwamba mtoto mchanga lazima anyonyeshwe kila baada ya saa tatu au nne.

Mpakate mtoto unapomnyonyesha. Kwa kumkumbatia mtoto anahisi mapenzi yako na inaweza kuathiri hata utu wake. Usimnyonyeshe mtoto mchanga wakati umelala chini kwa sababu imeonekana kwamba mama wengine hulala usingizi wakati wa kunyonyesha na matokeo yake watoto wengine wamekosa hewa kwa sababu matiti ya mama zao yaliwazuia kupumua.

Kama wewe mwenyewe huna maziwa kabisa unaweza kutumia maziwa ya ng’ombe ni mazito zaidi ya binadamu, pia lazima uongeze maji kiasi fulani. Pia unaweza kutumia maziwa yaliyosafishwa, ambayo lazima uyachemshe kwa muda wa dakika ishirini au hadi yanapokuwa salama kutumiwa na mtoto.

Usimnyonyeshe mtoto mchanga maziwa ya baridi au moto, lakini yanatakiwa yawe na joto sawa na yale ya binadamu.

Kila baada ya kunyonya lazima chupa na nyonyo zichemshwe kwenye maji na uangalifu wa ziada lazima ufanywe wakati wa majira ya joto. Uwe mwangalifu usitumie maziwa yaliyobakia au yaliyochacha. Ni vema kupima wingi wa maziwa katika kila kipindi cha kunyonya ili kuhakikisha kwamba mtoto wako anapata maziwa ya kutosha.

Katika kutumia maziwa ya unga unatakiwa upate ushauri kutoka kwa bingwa wa magonjwa ya watoto. Kila mara lazima utumie maziwa ya unga mapya.

Baada ya mwezi wa nne wa umri wa mtoto, unaweza kuanza kumyonyaesha maji ya matunda. Baada ya umri wa miezi sita, pia unaweza kuanza kumlisha vyakula vikavu na supu. Unaweza kumlisha bisikuti na mkate mtamu. Maziwa mtindi na jibini hufaa. Pole pole unaweza kuanza kumpa mtoto kiasi kidogo cha chakula chako.

Kumbuka kwamba mtoto wako mchanga huhisi kiu mara nyingi kama wewe. Kwa hiyo, mnyweshe maji, lakini sio chai au kahawa. Matunda, mboga na supu ni vyakula vyenye manufaa maalum kwa mtoto mchanga anayekua.

Usisahau kuwa safi kuhusu malazi ya mtoto, nguo zake na nepi zake. Mnawishe uso na mikono yake mara nyingi. Muogeshe katika vipindi vya kawaida, kwa sababu watoto wachanga ni rahisi sana kuugua kwa sababu ya uchafu na vijidudu.

Lazima watoto wapate chanjo ya kinga dhidi ya maradhi ya ndui, tetekuwanga, kifadulo, kiharusi cha watoto (polio), homa ya vipele

vyekundu, surua, dondakoo. Kwa bahati nzuri chanjo zipo zinapatikana kwenye hospitali na vituo vya afya kwa urahisi. Unaweza kuwa na watoto wenye afya njema kwa kushika kanuni za elimusiha na usafi.