پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Kupata Mtoto

Kupata Mtoto

Moja ya mambo ambayo huweza kuwa ni nukta zenye kuumiza kwa wanandoa ni kuhusu kupata mtoto.

Ni kwamba mwanamke atataka kupata mtoto lakini mume wake anakataa au kinyume chake. Tatizo hili wakati mwingine huwa kubwa sana na matokeo yake wanandoa wanaweza kuishia katika kutalikiana.

Bibi…alilalamika mahakamani na kusema: “Niliolewa nikiwa na umri wa miaka ishirini na saba ambapo mume wangu alikuwa amemaliza masomo ya Chuo Kikuu. Alikuwa mkufunzi kwenye mojawapo ya chuo kikuu na nilihisi kuwa nilikuwa mwanamke mwenye bahati. Hata hivyo mume wangu hataki kuzaa mtoto. Simwelewi kwa sababu sote afya zetu ni nzuri na tunazo fedha za kutosha kuwa na angalau watoto wawili. Si kwamba hawataki watoto, kwani anawatunza vizuri wapwa zake.

Nina umri wa miaka thelathini na kama ilivyo kawaida ningependa kuwa mama. Mume wangu anaelewa hisia zangu lakini husema kwamba mtoto atakuwa sababu ya usumbufu katika maisha yetu na kuendelea.” Mwanamke huyu, wakati anajizuia asilie, anakabiliwa na tatizo ambalo ni zito sana hivyo kwamba wanandoa hawa waliamua kutalikiana, ili yeye aweze kuolewa tena na mwanamume mwingine na yeye apate muda wa kutosha kufanya utafiti wake wa kisayansi.”

Kupenda watoto na kuzaa ni matamanio ya kawaida ya binadamu na hata ya hayawani. Watoto ni matunda ya maisha na urithi mzuri kuliko wote wa mwanadamu.

Maisha ya mtu mwenye watoto hayatasitishwa na kifo chake lakini, hakika yataendeshwa kama vile maisha yalivyo panuka. Mtu asiye na mtoto au watoto atahisi mpweke na aliye tupwa na atajihisi vibaya zaidi atakapo kuwa mzee.

Nyumba isiyo na watoto ni mahali panapo chosha na haitakuwa changamfu na upendo. Ndoa isiyo na watoto, wakati wowote ipo katika hatari ya kuvunjika. Hivyo watoto ni chanzo cha uchangamfu na kudumu kwa familia.

Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Furaha ya mtu imo katika kupata watoto.”

Mtume (s.a.w.) wa Uislamu alisema: “Zaeni watoto wengi kwa sababu mnamo Siku ya Hukumu nitajivunia idadi yenu juu ya umma nyingine.”

Kumpenda mtoto ni matamanio ya kawaida, lakini baadhi ya watu hupotoshwa kutoka kwenye kawaida yao na wanaathirika na maradhi ambayo huwafanya kutafuta visingizio kama vile upungufu wa fedha, kuwa ndio sababu ya kuwafanya wasipende kuzaa. Hata hivyo, Mwenyeyzi Mungu amehakikisha kwamba atawaruzuku viumbe Vyake vyote.

Bakr bin Saleh alisema: “Niliandika barua kwa Hadrat Abu al-Hasan (a.s) nikisema kwamba nilikuwa nachukua hatua za kuzuia nisipate mtoto kwa muda wa miaka mitano; kwa sababu mke wangu alikuwa anasita kupata mtoto, na kwamba alikuwa anasema kwamba ukosefu wa fedha ungefanya kazi ya kulea mtoto kuwa ngumu.’ Nilimuuliza Hadrat Abu al-Hasan maoni yake kuhusu jambo hili.” Akajibu: “Usizuie kupata mtoto, kwa sababu Mwenyezi Mungu Mweza atampa riziki.”

Mwenyezi Mungu Anaweza hata kuongeza riziki ya familia kwa sababu ya neema za watoto. Wapo watu wengi ambao walikuwa na shida kabla ya kupata watoto, lakini walipata maisha ya raha baadaye.

Baadhi ya watu huona watoto kama usumbufu. Hii si kweli na kwa kweli watoto ni chanzo kizuri sana cha furaha na kiburudisho kwa wazazi.

Kama ilivyo, kutunza watoto si kazi rahisi na yenye matatizo, lakini maadam inaafikiana na kanuni ya asili, mtu anaweza kuvumilia matatizo na kwa hali hiyo inafaa kukubali usumbufu uliomo humo.

Ufinyu ulioje wa akili wa wanaume na wanawake ambao kwa sababu ya kutokupata watoto wanakimbilia kuachana! Je si kweli kwamba inashangaza mwanaume mwenye elimu, anakataa kukubali sheria za utaratibu wa jambo la asili kwa kung’ang’ania kiasi cha hata kuwa tayari kumpa talaka mke wake?

Wanandoa wengine hukubaliana kupata mtoto lakini hubishana kuhusu wakati wa kupatikana mtoto. Mwanamke au mwanaume wa aina hii angesema; ‘Mtu lazima awe huru wakati wa umri mdogo kwani mtoto atamnyima uhuru wa kustarehe.

Ni vema kungoja hadi baadaye kupata mtoto mmoja au wawili.’ Kama wote mume na mke wanatofautiana kwa maoni, basi mabishano yataanza ambayo yanaweza kuishia kwenye kutalikiana.

Na tukumbuke kwamba kama mtu anataka watoto, basi lengo hili lingetekelezwa katika kipindi cha mwanzo kabisa cha ndoa. Hii ni kwa sababu watoto wanaozaliwa na wazazi vijana kwa kiasi fulani huwa bora kuliko wale wanaozaliwa na wazazi wenye umri mkubwa zaidi. Kwanza, watoto hawa afya zao huwa njema zaidi na wanaonekana kuwa na nguvu nyingi zaidi. Pili, kwa kuwa wanatokana na wazazi vijana, wanaweza kuishi kwa muda mrefu zaidi na wazazi wao. Wanaweza kusomeshwa zaidi na kulelelewa vizuri zaidi. Lakini watoto walio zaliwa na wazazi wenye umri mkubwa hunyang’anywa uongozi na mafundisho ya wazazi wao kwa sababu ya kifo au kukosa uwezo. Tatu watoto wa wazazi wenye umri mdogo wangeweza kufika kwenye umri wa kuwa na familia zao na kuanza kufanya kazi, ambapo wazazi wao wakingali hai. Hivyo wanaweza kuwa msaada mkubwa sana kwa wazazi wao watakapo kuwa wazee.

Kwa ufupi, kuzaa watoto wakati wa ujana ni vema zaidi kuliko umri mkubwa. Lakini hiki si kipengele cha muhimu sana hivyo kwamba kisababishe ugomvi na kutalikiana. Ni vema kwa mwanaume au mke kukubaliana kwa maelewano wasiruhusu suala hili kutengeneza mwanya katika ndoa yao.

Baadhi ya wanandoa hushindwa kuelewana kuhusu idadi ya watoto ambao wangetaka kuzaa.

Mwanamke akiwa amemshikia mtoto mikononi mwake alisema: “Miaka minne baada ya kuoana, nilizaa watoto wa kike wawili na mume wangu, lakini kwa kuwa alitaka mtoto mwanaume, nilipata ujauzito kwa mara nyingine na tena nilijifungua mtoto mwanamke. Sasa ninao watoto watatu wanawake. Mume wangu anafanya kazi benki na mshahara wake hautoshi familia yetu. Hivi karibuni amekuwa akisisitiza kwamba nibebe mimba mara nyingi hadi nizae mtoto wa kiume. Lakini mimi sipo tayari kwa mpango huu kwa sababu kipato chake hakitoshi kuwasomesha watoto wetu kwa namna tunavyotaka. Nimemwambia mara nyingi kwamba watoto wanaume na wanawake wote ni wazuri. Nina hofia kwamba kama nikibeba ujauzito tena nitazaa mtoto mwanamke tena.

Nina uhakika kwamba atataka kusisitiza tupate mtoto mwingine. Hatutakubaliana katika jambo hili na hivyo tumeleta shauri letu mahakamani.”

Ni sahihi kwamba kusomesha na kuelekeza watoto wengi ni vigumu na hii hususan ni kweli wako ambao hawana kipato cha kutosha.

Kwa hiyo, ni vema wanandoa kuamua kuhusu idadi ya watoto kwa mujibu wa kimaadili na uwezo wa kifedha. Lazima waelewane na waweze kupata ufumbuzi wa matatizo yao kwa kutumia busara na wema. Si sahihi kwa yeyote miongoni mwao kusisitiza kitu kisicho na mantiki.

Zipo familia nyingi ambazo ama wanao watoto wengi au zinatosheka na mtoto mmoja au wawili.

Baadhi ya wanandoa hutofautisha kuhusu jinsia ya mtoto (watoto) wanaotaka kuzaa. Wanandoa wengine, wanaume na wanawake hupenda kuzaa mtoto mwanaume na hawapendi kuzaa watoto wanawake. Kuzaliwa kwa mtoto mwanamke ni tukio ambalo lingemfanya mzazi mwanamke ajihisi ana hatia na kwa hiyo angenyamaza kwa sababu ni yeye ndiye amezaa. Lakini mwanamume huenda akaonesha kutokuridhika kwake. Wanaume wapo tofauti. Baadhi yao hawaoneshi kutokuridhika kwao wazi wazi na huishia kuonesha tu uso wa kuogofya. hawatilii maanani kuwahudumia wake zao baada ya kujifungua. Huonekana na huzuni.

Baadhi ya wanamume, hata hivyo huwa wakali sana wanapopata taarifa ya kuzaliwa mtoto wa kike. Huwakasirikia wake zao na huanzisha shutuma za makosa yao. Hupinga na kuanzisha ugomvi. Wanaume wengine huamua hata kuwapiga wake zao au kuwataliki.

Mwanamke alisema mahakamani; “Niliolewa miezi kumi na tano iliyopita na nikapata ujauzito miezi sita baadaye. Hivi karibuni, muda wa kujifungua ulipokaribia, mume wangu aliniambia kwamba nizae mtoto mwanaume. Lakini nilihisi kwamba ningezaa mapacha au hata watatu. Siku chache zilizopita nilijifungua mapacha wa kike. Nilifurahi sana kuhusu jambo hili, alitibuka na akaondoka hapo chumbani. Baadaye nilimuomba awapeleke watoto nyumbani, alinikaripia na kunilaumu kwa kuzaa mapacha wanawake. Akaniambia niondoke kwake, kwa hiyo nilikwenda kwa wazazi wangu na sasa ninaomba anipe talaka.”

Bibi… alimwambia mwandishi wa habari mahakamani: “Baada ya miaka ishirini na moja ya ndoa na kuzaa watoto watano, ninalazimika kuyaacha maisha ambayo nimeyapatia mchango mkubwa sana, kwa kumpisha mwanamke mwingine ambaye ameweza kuzaa mtoto mwanaume.

“Ninao watoto wanawake watano wazuri ambao ni wenye vipaji na ambao si tatizo kabisa kwa baba yao. Ni ipi hatia yangu kama siwezi kuzaa mtoto wa kiume. Mume wangu ananilaumu kwa kutokuzaa mtoto wa kiume na anataka mimi nimruhusu kuoa mwanamke mwingine.”

Kwa bahati mbaya, sifa hii imeendelezwa na watu wengine tangu enzi za Ujahiliya (kipindi cha ujinga) kwamba hutilia shaka maumbile ya binadamu ya jinsia ya kike. Huoni aibu kuzaa watoto wa kike na huhisi wamedhalilishwa.

Katika zama zaa ujinga, watu walikuwa na desturi ya kuzika watoto wa kike wakingali hai! Qurani Tukufu imesema kuhusu matendo yao ifuatavyo:


وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُمْ بِالْأُنْثَىٰ ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ کَظِیمٌ

“Na mmoja wao akibashiriwa kwa msichana, uso wake unasawijika, naye kajaa chuki.” (Quran 16:58)

 

یَتَوَارَىٰ مِنَ الْقَوْمِ مِنْ سُوءِ مَا بُشِّرَ بِهِ ۚ أَیُمْسِکُهُ عَلَىٰ هُونٍ أَمْ یَدُسُّهُ فِی التُّرَابِ ۗ أَلَا سَاءَ مَا یَحْکُمُونَ

“Anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa aliyo bashiriwa! Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama uovu wa wanavyohukumu!” (Quran 16:59).
Lakini Uislamu unapinga fikira hii isiyo sahihi na kuwaona wanawake na wanamume kuwa wapo sawa.

Mtume (s.a.w.) wa Uislamu alisema: “Miongoni mwa watoto wenu walio bora zaidi ni mabinti zenu.”

Mtume (s.a.w.w) wa Uislam pia alisema: “Ishara ya mwanamke mwenye bahati ni yule ambaye mwanaye wa kwanza ni mwanamke.”

Kwa nyongeza, Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Yeyote ambaye anawalea watoto wanawake watatu au dada watatu, Pepo itakuwa ya kwake.”

Kama mtoto mwanamke angekuwa duni, Mwenyezi Mungu hangefanya ukoo wa Mtume (s.a.w.) uendelee kupitia kwa Hadhrat Fatima Zahra (a.s).

Bwana mpendwa! Unadai kwamba wewe ni mstaarabu na binadamu wa kisasa, kwa hiyo acha fikira za aina hiyo. Kuna tofauti gani wewe ukiwa na mtoto mwanamke au mwanamume. Wote hawa ni watoto wako na wote waweza kuelekea kwenye ubora. Mtoto mwanamke pia anaweza kuwa mtu mashuhuri kwa malezi yako sahihi ya elimu. Mtoto mwanamke ni bora zaidi ya mtoto mwanamume kwa kiasi fulani:

Kwanza, mtoto mwanamke ana huruma zaidi kwa wazazi wake anapokua na kujitegemea. Watoto wanawake, kama wazazi hawawapi upendeleo wowote zaidi ya watoto wao wanamume, wangekuwa na mapenzi zaidi kwao.

Pili, mtoto mwanamke mahitaji yake hayana gharama kubwa kama ya mtoto wa kiume, kwa sababu kwa kawaida hadumu muda mrefu nyumbani kwa wazazi wake, kwani huolewa mapema katika umri wake na huwaacha wazazi wake akiwa na vitu vichache tu vya kuanzia maisha yake mapya. lakini, wavulana huwa wa makamo ya vijana ambao huweza kuishi na wazazi wao kwa muda mrefu. Wazazi watalipa gharama ya elimu yake, wtamtafutia kazi, watalipa gharama zake wakati wa miaka miwili ya kutumikia jeshi, kama upo umuhimu, na halafu kumuoza mke, baada ya hapo angehitaji kupewa nyumba, mabusati, samani, na kadhalika. Angehitaji hata msaada wa fedha kutoka kwa wazazi wake baada ya kuoa.

Tatu, kama wazazi hawatafanya ubaguzi baina ya mtoto wao mwanaume na mwanamke, na kama watamtendea wema mkwilima wao, mkwilima wao mara nyingi huenda akawasaidia wao wakati wa matatizo na kwa kawaida huwa mwaminifu zaidi kwao kulinganisha na mtoto wao wa kiume.

Kwa vyovyote vile, hivi huwa ni kosa la mwanamke inapotokea anazaa mtoto mwanamke?

Mume na mke wote wanahusika katika tendo la kuzaa na mwanaume hana haki ya kumlaumu mke wake kwa jambo hili. Vinginevyo ni sawa kabisa mwanamke naye kumlaumu mume wake kuhusu jambo hili. Hata hivyo, hapana yeyote kati yao anaye laumiwa kwa jambo hilo kwani ni utashi wa Allah pekee wenye kuamua jinsia ya mtoto.

Wapo baadhi ya wataalamu ambao wanaamini kwamba jinsia ya mtoto inaweza kuamuliwa kutokana na jinsi mama anavyopata lishe yake wakati wa ujauzito wake. kwa hiyo, kama wapo watu wanaopendelea mtoto wao awe na jinsia wanayotaka wao, wanaona wataalamu na kwa hiyo watazuia hali ya kuwalaumu wake zao.

Mtu mwenye akili si lazima afadhaike kwa kupata mtoto mwanamke, lakini lazima afurahi sana. Anatakiwa kuonesha furaha yake, huba yake kwa mke wake na anatakiwa hata kumpa mke wake zawadi.

Angeweza kusherehekea kupatikana kiumbe kipya na hata kuchukua hatua za kimantiki katika kumridhisha mke wake kwamba mtoto mwanamke ni bora kama alivyo mtoto mwanaume, iwapo mke wake atakuwa amefadhaika kwa sababu ya kupata mtoto mwanamke.

Baba mwenye busara hawezi kubagua baina ya mtoto wake mwanaume na mwanamke, hangemlaani yeyote kwa kupata mtoto mwanamke na kwa hiyo angepambana na fikira za kipindi cha ujahiliya.

Mwanaume alisikia habari ya kuzaliwa mtoto wa kike wakati alipokuwa na Mtukufu Mtume wa Uislamu (s.a.w.w). taarifa hiyo ilimvuruga. Mtume

(s.a.w.w) alisema: “Kwa nini umefadhaika?” Alisema: ‘nilipokuwa ninatoka nje ya nyumba yangu, mke wangu alikuwa katika uchungu wa kujifungua, na sasa nimeletewa taarifa kwamba nimepata mtoto mwanamke.’ Mtume (s.a.w.w) alisema; “Ardhi inayo nafasi ya kumtosha yeye, na mbingu inampa hifadhi na Mwenyezi Mungu atampa riziki. Yeye ni ua lenye kutoa harufu nzuri ambamo kutoka humo utapata furaha kubwa.”