پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Uchumi Wa Familia

Uchumi Wa Familia

Kufanya mpango wa sadaka ya mke ni wajibu wa mume. Ni kwamba mwanaume anawajibika kulipa gharama za mke wake kama chakula, nguo, nyumba, daktari na dawa. Atakuwa anakosea kama hata mgharimia mke wake na anaweza kushitakiwa kisheria.

Mtu hawezi kutarajia familia iishi bila matumizi yeyote ya fedha. Watu wa familia wote wanahitaji chakula, nguo, dawa na mahali pa kuishi. Hata hivyo, wanaweza wakaomba vitu visivyo muhimu ambavyo mwanaume anaweza kukataa kuvinunua na asikubaliane na matakwa yao mbali mbali.

Mtu mwenye busara atatumia fedha kufuatana na uwezo wa kipato chake. Lazima abainishe bidhaa muhimu na avinunue katika mpango wa kipaumbele wakati wowote anapoweza. Lazima pia aweke akiba ya fedha kwa matumizi ya siku za shida. Kiasi fulani cha fedha lazima kitengwe kwa ajili ya kodi ya nyumba au kununua mahali pengine. Lazima mume asisahahu umeme, maji, nishati na simu. Kodi na ada za shule lazima zikumbukwe. Lazima kabisa aepukane na kutumia zaidi ya bajeti na kulipa vitu visivyo muhimu. Mpango mzuri wa matumizi ya fedha utamwepusha mtu asifilisike au kuwa na madeni.

Mwenyezi Mungu huona matumizi yaliyopangwa vizuri ni ishara ya imani na anasema ndani ya Qurani:


وَالَّذِینَ إِذَا أَنْفَقُوا لَمْ یُسْرِفُوا وَلَمْ یَقْتُرُوا وَکَانَ بَیْنَ ذَٰلِکَ قَوَامًا


 

“Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili bali wanakuwa katikati baina ya hayo”. ( Quran 25:67).
Imamu Sadiq (a.s) alisema: “Yapo makundi manne ya watu ambao sala zao hazitafika kiwango cha kukubaliwa; Kundi moja ni la watu ambao hutumia vibaya utajiri halafu humwomba Mwenyezi Mungu Mweza, ‘Ee Mwenyezi Mungu naomba riziki. Halafu Mwenyezi Mungu hujibu, si nilikuagiza uwe mwangalifu katika matumizi yako. ’ ”

Abdullah bin Aban anasema: “Nilimuuliza Musa bin Jafar (a.s) kuhusu utunzaji wa familia ya mtu na akasema: ‘Ubadhilifu na uchoyo vyote ni sifa mbaya. Mtu lazima awe na kiasi.”

Mtu mwenye busara ataepuka kukopa fedha na hawezi kuchukua mkopo kwa matumizi mabaya. Uchumi unaotegemea mikopo (na riba), inayopokewa kutoka kwenye mabenki na taasisi zingine si sahihi kiislamu na kimantiki haufai.

Kununua vitu kwa mkopo, ingawa hufanya nyumba yako ionekane nzuri, lakini faraja na utulivu wa akili hutoweka.

Kwa nini mtu ananunua vitu visivyo muhimu kwa bei ya juu zaidi na kujaza mifuko ya wenye mabenki kwa malipo kidogo? Ni maisha ya aina gani hayo ambapo kila kitu hupatikana kwa bei ya mkopo? Kwani si vema zaidi kwa mtu kungoja na kuweka akiba ili anunue bidhaa kwa bei nafuu?

Ni kweli kwamba kupata fedha ni vigumu na huathiri sana maisha ya mtu. Hata hivyo, la muhimu zaidi ni jinsi mtu anavyotumia fedha yake. Zipo familia zenye vipato vizuri ambazo kila mara ni wadeni wa wengine. Zipo pia familia nyingi zenye vipato vya chini ambao huishi kwa raha. Tofauti baina ya makundi haya mawili ni jinsi ya fedha inavyo tumiwa. Kwa hiyo, inafaa zaidi ama mwanaume aendeshe udhibiti wa matumizi au awe msimamizi wa mtu ambaye anawajibika nayo.

Mwisho, inakumbushwa kwamba ubakhili ni mbaya kama ufujaji, kama mwanaume anacho kipato zaidi lazima aifurahishe familia yake zaidi na kuwapa mahitaji yao muhimu kadiri iwezekanavyo.

Utajiri na fedha vyote ni vya kutumia na kuwezesha upatikanaji wa vitu muhimu vya maisha, na si vya kulundika na kuviacha hapa duniani.

Ishara za utajiri lazima zionekane wazi kwenye familia ya mtu na nyumba. Kuna manufaa gani kufanya kazi kwa bidii halafu kinachopatikana kisitumike?

Mtu mzima atumie utajiri kuhusu familia yake na starehe yake mwenyewe. Inachukiza kuona mtu ambaye anao uwezo wa kifedha lakini watoto wake wanatamaani chakula kizuri na nguo nzuri. Watoto wa mtu bakhili kungoja kifo chake ili wagawane utajiri wake. Kama Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anampa mtu neema zake, neema hizi lazima zidhihiri katika maisha ya mtu huyo.

Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu alisema: “Si mwenzetu (si mfuasi wa Mtume s.a.w.w) ambaye anazo fedha lakini huiweka familia yake mbali na utajiri wake.”

Musa bin Jafar (a.s) alisema: Jamaa ya mtu ni watu wanaomtegemea. Hivyo, yeyote anayepewa neema za Mwenyezi Mungu, lazima azisambaze kwa wale wanao mtegemea ili wafarijike, au vinginevyo neema hizo zitaondoshwa kwake.”

Imamu Rida (a.s) alisema: “Ni jambo la manufaa kwa mtu kuwapa watu wa familia yake starehe itokanayo na matumizi yake, ili wasingoje hadi hapo atakapofikwa na mauti.”

Imamu Ali (a.s) alisema: “Tayarisha matunda kwa ajili ya watu wanaokutegemea kila siku ya Ijumaa ili kwamba watafurahia kuja kwa Ijumaa.”