Talaka

Talaka

Licha ya kwamba talaka ni kitendo halali, ni kitendo kinacho chukiza na ni kibaya kuzidi vitendo vyote.

Imam Sadiq (a.s) alisema: “Oeni lakini msitalikiane, kwa sababu talaka inaweza kutetemesha Arsh ya Mwenyezi Mungu.”

Imam Sadiq (a.s) pia alisema: “Mwenyezi Mungu huipenda nyumba ambayo inakaliwa na wanandoa na huchukia nyumba ambayo wanandoa wametalikiana. Hakuna kitendo kinacho mchukiza Mwenyezi Mungu kuliko kutalikiana.”

Ndoa si kama kununua jozi ya viatu au soksi ambapo vitu hivi vikichujuka kwenye matamanio ya mmiliki wake, huvitupa na kununua jozi nyingine ya viatu. Ndoa ni makubaliano ya kiroho ambayo hufanywa na watu wawili kwa lengo la kuishi pamoja kama marafiki wa kuliwazana, na wapenzi hadi kifo chao. Makubaliano haya yameegemezwa kwenye matumaini haya hivyo kwamba msichana huwaacha wazazi wake na kuungana na mume wake.

Mwanaume hufanya jitihada na kufanya bidii kwa msingi wa makubaliano hayo ya kimungu. Hulipa gharama za harusi yake na hununua vitu muhimu kwa ajili ya maisha yake mapya na hufanya kazi kwa ajili ya faraja ya familia yake.

Ndoa si jambo la kukata kiu cha tamaa ya kimwili na wanandoa hawawezi kuiharibu kwa visingizio vidogo. Licha ya kwamba kutalikiana ni tendo halali, linachukiza sana na watu wanashauriwa kuepukana nalo kadiri iwezekanavyo.

Bahati mbaya, tendo hili ambalo linachukiza sana, limekuwa jambo la kawaida sana kwenye nchi za kiislamu na misingi ya familia imetikisika sana, hivyo kwamba kwa ujumla watu hawana imani tena kuhusu ndoa.

Kuvunja ndoa inaruhusiwa hapo tu ambapo hali si ya kawaida na inalazimu iwe hivyo.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Malaika Jibril aliniusia kuhusu wanawake sana hivyo kwamba nilifikiri kwamba wanamume wasiwataliki isipokuwa kama wanazini.”

Kesi nyingi za kutalikiana hazina sababu za msingi, isipokuwa visingizio visivyo komaa. Yaani, sababu za kesi nyingi zaidi za talaka ni hafifu na hazifai kuwaathiri na kuwatenganisha wanandoa. Mume au mke, kwa sababu ya ubinafsi, anaweza kukuza jambo dogo na kuamua kwamba maisha yao ya ndoa lazima yakome.

“Bibi fulani mwenye umri wa miaka ishirini na nne, alimwambia mumewe awaalike wazazi wake kwenye chakula cha jioni chenye gharama kubwa. Kwa kuwa hakutekelezewa ombi hilo, alidai talaka.”

“Mwanaume alimtaliki mke wake kwa sababu alikuwa anazaa watoto wanawake tu. Wanandoa hawa walikuwa na watoto wanawake watano.”

“Mwanamke aliomba talaka kwa sababu mume wake aliamini mafundisho ya kumfikiri Mungu kwa njia ya tafakuri na hakuonesha kupenda maisha.”

“Mwanamume alidai talaka kwa sababu alitaka kumuoa mwanamke tajiri.”

“Mwanamke aliomba talaka kwa sababu mume wake alikuwa na tabia ya kuficha fedha zake kwenye mikono ya shati.”

“Mwanaume alimtaliki mke wake kwa madai kwamba ana balaa tangu walipooana baba wa mume alifariki na ami yake alifilisika.”

Wanandoa ambao hawana heshima na busara, wanaweza wakanasa kwenye mtego wa mambo madogo kama hayo na kudai talaka.

Wanandoa wanaotaka kutengana, wasifanye haraka kutelekeza jambo hilo. Wanashauriwa wafikiri kwa uangalifu kuhusu athari na maisha yao ya baadaye kwa makini na halafu waamuwe. Hususan lazima watafakari kuhusu mambo mawili:

Jambo la kwanza: wanandoa wanaotaka kutalikiana kwa kawaida hutaka kuoa au kuolewa tena. Lakini lazima wakumbuke kwamba baada ya kutalikiana, watu wanaojulikana kama watalaka hawatakuwa na sifa nzuri kuhusu ndoa. Watu huwafikiria kuwa wenye ubinafsi na si waaminifu.

Baada ya kupata taarifa ya maisha ya ndoa ya siku za nyuma ya mwanamume na kutaliki, mwanamke anaweza kuwa na shaka kuhusu uaminifu wa mwanaume au tabia yake.

Mwanamke mtalaka ni nadra sana kupata fursa ya kuolewa tena. Kwa sababu wanaume kwa kawaida hawaoneshi kuvutiwa sana kuoa mwanamke mtalaka na hutilia shaka kuhusu uaminifu wake.

Kwa hiyo, mtalaka anawezekana akaishi peke yake kwa muda wote wa maisha yake na atateswa na upweke pia.

Kuwa mpweke ni hali ngumu sana na watu wengine wapweke hupendelea zaidi kifo kuliko maisha ya aina hiyo yasiyovumilika.

Mwanamke wa miaka ishirini na mbili ambaye aliachika, alijaribu kujiua mnamo usiku wa siku ya harusi ya dada yake. Alikuwa na mtoto mmoja.

Hata kama mwanaume anafaulu kuoa tena, haitajulikana kabisa kwamba maisha yake mapya yatakuwa mazuri zaidi kuliko ya mke wake wa mwanzo. Mke wake wa pili anaweza kuwa mbaya zaidi. Mwanaume wa aina hii hupendelea kumtaliki mke wa ndoa ya pili na kurudi kumuoa mke wa kwanza. Lakini kwa kawaida huwa wamechelewa sana.

Mwanaume wa miaka themanini alisema mahakamani; “Nilikuwa na maisha mazuri nilipomuoa mke wangu wa ndoa ya kwanza, takriban miaka sitini iliyopita. Lakini baada ya muda alianza kunifanyia ubaya kwa hiyo nikamtaliki. Nilioa wanawake wachache baada ya hapo lakini nilihisi kwamba mke wangu wa kwanza alikuwa mwaminifu zaidi miongoni mwao. Nilimuona na nikampa rai ya kurudiana naye. Yeye, ambaye pia alichoka maisha ya upweke alikubali na sasa tunataka kuoana tena.”

Mwanaume alimtaliki mke wake wa pili kwa sababu hakutaka kuwalea watoto wawili aliozaa kwenye ndoa yake ya kwanza. Halafu akaamua kumuoa tena mke wake wa kwanza ambaye alimtaliki miaka mitano ya nyuma.’ Jambo la pili: Wanandoa ambao wanataka kutengana lazima wafikirie pia suala la watoto wao. Faraja ya watoto imo kwenye familia yenye wazazi wote wanao ishi pamoja na wanawalea kwa pamoja.

Baada ya kuvunjika kwa maisha ya familia, watoto hufadhaika sana. Kama ni baba yao tu anaye watunza, hawatakuwa na maisha na mama yao wa kambo. Mama wa kambo si tu kwamba wanashindwa kutekeleza kama mama halisi, lakini wanaweza kufikiri watoto wa kambo ni mzigo. Mama wa kambo wengine huwanyanyasa watoto wa kambo na kuwafadhaisha kwa kukusudia na baba zao hunyamaza kimya.

Bibi harusi wa miaka kumi na nne ambaye alitaka kujiua alisema akiwa hospitalini. Wazazi wangu walitengana nilipokuwa na mwaka mmoja.

Baba yangu alioa tena baada ya mwaka mmoja na nusu na sasa tunaishi wote. Mama yangu wa kambo alikuwa na desturi ya kunipiga na hata alinichoma moto kwa chuma mara kadhaa. Baba yangu licha ya kuwa na uwezo wa kifedha alinikataza nisisome. Takriban mwezi mmoja uliopita baba yangu alinioza kwa mtu mwenye umri wa miaka arobaini na tano.

Msichana wa miaka kumi na tatu alijinyonga. Msichana huyu aliishi na kaka zake wawili. Mmojawapo wa hao kaka zake alisema; “Wazazi wetu walitengana miaka takriban mitatu iliyopita. Mama yangu aliolewa tena na mwanamume mwingine na baba alikufa miezi miwili iliyopita. Ilikuwa saa 12:30 jana jioni nilikuja nyumbani nikamkuta dada yangu amejinyonga.”

Pia, kama mama anachukua wajibu wa watoto wake, basi watakosa baba halisi ambaye angewatunza. baba wa kambo mara nyingi ndiye sababu ya kukosekana furaha kwa watoto wake wa kambo.

Mwanamke alimsaidia mume wake wa ndoa ya pili kumfunga mtoto wa kambo mwenye umri wa miaka nane kwenye kitanda. Halafu wakafunga mlango na wakaondoka kwenda matembezini. Waliporudi nyumbani,walikuta mtoto wao ameungua moto hadi kufa kwa sababu ya moto uliounguza nyumba.

Talaka huharibu familia na huwaacha watoto wanatangatanga hawana hifadhi. Watoto mara nyingi huteseka kwa sababu ya ubinafsi wa wazazi wao.

Watoto wanne wenye umri wa miaka kumi na mbili, tisa, sita na minne walikwenda kwenye kituo cha polisi. Mtoto mwanamme mwenye umri mkubwa zaidi alisema: “Wazazi wetu walitengana muda fulani uliopita. Wakati wote walikuwa wanabishana na walikuwa na tabia ya kugombana kila siku mchana na usiku. Sasa wametalikina, hapana mmojawao ambaye yupo tayari kutulea sisi.”

Watoto ambao hawana mlezi anayefaa na mazingira ya familia, mara nyingi hukengeuka. Kutokupata elimu ya kutosha na mtu mwenye huruma katika maisha yao, huwafanya wasumbuliwe na hisia za udhalili. Wanaweza hata kufanya uhalifu wa viwango mbali mbali, wakati wa utoto au utu uzima.

Mtu anaweza kutambua jambo hili na kusoma matukio kwenye magazeti kila siku.

Kwenye utafiti uliofanywa kwenye kituo cha kurekebisha vijana, ni wazi kwamba katika vijana wahalifu mia moja kumi na sita wa kituo hiki, watu themanini walithibitisha kwamba mama zao wa kambo waliwanyanyasa ndio sababu wakafanya uhalifu.”

Mpendwa bibi na bwana! Kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya watoto wako wasio na kosa, kuweni wasamehevu nyinyi kwa nyinyi wanandoa. Msikuze matatizo madogo na msipende kung’ang’ania ubishi. Msitafutane makosa nyinyi kwa nyinyi. Fikirieni mambo yenu ya siku zijazo na watoto wenu.

Kumbukeni watoto wenu wanawategemeeni nyinyi na wanatumaini kupata furaha yao kutoka kwenu. Wahurumieni na msiharibu maisha yao.

Kama mkidharau matamanio yao ya ndani na kama mkivunja nyoyo zao ndogo, hamtaweza kuepuka athari ya masikitiko yao. Kwa hiyo, hamtaweza kuwa na maisha yenye faraja pamoja.