پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Puuza Mazungumzo Ya Uongo Ya Wakosoaji

Puuza Mazungumzo Ya Uongo Ya Wakosoaji

Baadhi ya watu wanayo mazoea ya kuwazushia uongo watu wengine. Tabia hii isiyo pendeza hutengeneza uadui miongoni mwa marafiki, na ndugu na inaweza kuvunja familia. Imeweza hata kusababisha mauaji. Zipo sababu mbali mbali kuhusu tabia ya aina hii, kama wivu, hasira, kisasi na uadui.

Baadhi ya watu hukimbilia kutamka maneno ya kashifa ili waridhishe nafsi zao. wasikilizwe na watu wengine au kujifanya wanamuonea huruma mtu fulani. Lakini ni mara chache sana kwamba maneno ya kashifa huwa na makusudio mazuri.

Kwa hiyo, mtu mwenye hekima na mjanja anatakiwa kupuuza maneno kama hayo. Lazima afanye uchambuzi wa maneno ya msemaji kila mara ili aepuke kudanganya au kuvutiwa na uovu wake wa masingizio.

Jambo moja ambalo wanamume wanatakiwa kukumbuka ni kwamba kwa kawaida mama zao, dada zao, kaka zao, licha ya kuonesha urafiki, huwa hawafurahii uhusiano mzuri na wake zao.

Sababu ni kwamba, kabla ya kuoa mwanaume huishi na wazazi wake kwa miaka mingi ambapo huwa hana uhuru wa kutosha. Wazazi wake ambao wamefanya bidii kumlea wanayo matarajio ya kupata msaada kutoka kwake pindi wanapofika kwenye umri wa uzeeni.

Wazazi hata baada ya kumuoza mtoto wao wa kiume na kumpa uhuru bado wanayo matumaini kwamba atafuata ridhaa yao na matakwa yao. Hupenda mtoto wao wa kiume kuwatunza wao zaidi kuliko mkewe. Lakini ukweli ni kwamba, mwanaume anapoanza maisha ya ndoa, hujitahidi sana kwa ajili ya familia yake mpya, mke na kujitegemea.

Huelekeza mapenzi yake kwa mke wake na hufanya bidii kuhusu lengo hilo. Jinsi anavyozidi kuingia upande wa ndoa, ndivyo anavyozidi kuwa mbali na wazazi wake.

Hivyo mama yake na dada zake hususan hujihisi wamekosewa. Humuona bibi harusi kama tishio kwao kwani atakuwa amemchukua kijana wao kutoka kwao. Inawezekana wamlaumu bibi harusi kwa kumtenganisha kijana wao kutoka kwenye familia yake.

Wakati mwingine mama wa waume hudhani kwamba njia iliyo nzuri sana ya kukabiliana na hatari hii ni kutekeleza njia za kusababisha watoto wao (waume) wapunguze huba kwa wake zao.

Mama wa aina hii, ataanza kuonesha mapungufu ya mke wa mwanae, kutangaza uongo kuhusu bibi harusi, kusema maneno ya kashfa na kufanya njama dhidi ya muolewaji na kadhalika. Kama mwanaume anadanganyika kwa urahisi na mjinga, inawezekana akakubaliana na maneno ya kashifa ya mama yake. Hapo sasa mume atakuwa kitendea kazi kilichomo mikononi mwa familia yake ambapo matokeo yake baadaye atapoteza mvuto kwa mkewe. Akiwa kwenye ushawishi wa wazazi wake mwanaume ataanza kulalamika na kuonesha makosa ya mke wake. Atamlaumu mke wake wakati wowote itakapo wezekana.

Matokeo yake, nyumba ya familia itageuka kuwa baridi na isiyopendeza. Uchochezi wa wanaume kutoka kwa mama na dada zao huwaelekeza wanandoa kwenye ugomvi na hata kupigana. Katika hali hii, mke anaweza kukimbilia kuchukua hatua kali zaidi kama kujiua!

Mwanamke ambaye alikuwa katika siku zake za mwanzo wa ndoa, alimeza pini.

Baada ya kufanyiwa upasuaji kwa lengo la kuondoa pini kutoka tumboni mwake, alisema; Kama juma moja hivi lililopita, niliolewa. Siku nilipoingia nyumbani kwa mume wangu, nilihisi kuwa na bahati kama wanawake wengine walioolewa. Lakini baada ya siku chache tu, mume wangu na dada yake walianza kunilaumu. Msimamo wao ulifanya maisha yangu kuwa magumu sana. Hatimaye niliamua kujiua na nikameza pini chache.”

Mwanamke ambaye alikasirishwa na lawama za mume, shemeji yake, alijichoma moto na kufa kwa sababu ya majeraha makali.”

Mwanamke ambaye alikuwa katika siku zake za mwanzo za kuolewa aliudhiwa sana na msimamo mbaya wa mama mkwe wake hivyo kwamba alijichoma moto hadi kufa.”

Kwa hiyo, lawama, msimamo mbaya na maneno ya kashfa kutoka kwa mama, dada na kaka zao waume ni tabia ambazo zinaweza kuwa na madhara makubwa sana na hivyo mwanaume lazima atahadhari kuhusu usumbufu wao. Kama mambo yalivyo, haiwezekani kuwazuia watu wasiseme lakini inawezekana kutangua mazungumzo yao.

Mwanaume lazima atambue kwamba lawama zinazo elekezwa kwa mke wake na mama yake, dada zake na kadhalika hazina maana ya kuhurumiwa na kuwa na nia njema, isipokuwa sababu kubwa ni wivu, uadui uchoyo na kadhalika.

Mwanaume lazima akumbuke kwamba kwa sababu ya mke kwa kufanya uzingativu wa mume wake uelekee kwake, familia yake humuonea wivu na kumchukulia kama mporaji wa kijana wao. Kwa hiyo, hukimbilia kutumia njia za kuzuia mapenzi yao yasisitawi.

Mabwana wapendwa kwa ufupi, mama, dada na kaka zenu wa aina hii hawajali furaha yenu katika ndoa, lakini hususan wao wanaangalia matakwa yao. Kama wangekuwa wanahusika na furaha yako na mke wako wangefanya vinginevyo.

Ni jambo la kushangaza kwamba wazazi hutoa sifa nyingi sana kwa mwanamke anayetarajiwa kuolewa na mtoto wao wa kiume, lakini mara mtoto wao anapooa wazazi hao hugeuka na kuwa kinyume.

Mabwana wapendwa msidanganywe. mapungufu hayo ambayo familia yako huyapachika kwa mke wako hayana umuhimu wowote; na hata kama si madogo, kumbuka kwamba hakuna mtu aliye kamilika.

Kwa vyovyote vile, je, dada na mama yako au wengine wanao mlaumu mke wako, wao ni viumbe vilivyo kamilikia?

Kuzingatia maneno yao ya kashfa ni hali ambayo itaathiri maisha ya familia yako. Inawezekana ukaishia kuachana, na matokeo yake ni kwamba unaweza kuteseka kiakili na kiuchumi.

Kuoa mara nyingine haitakuwa rahisi. Hata kama utapata mwanamke mwingine wa kuoa, haileweki kabisa kwamba atakuwa mkamilifu kuliko yule wa kwanza. Utahakikishaje kwamba familia yako hawatamtendea vibaya kama walivyofanya kwa mkeo wa kwanza?

Kwa hiyo, ni vema umwambie mama yako, dada yako na wengine kuanzia sasa kwamba mke wako anakufaa na kwamba unampenda. Lazima uwatangazie kwamba lazima waache kumlaumu mke wako au vinginevyo mke wako au wewe mwenyewe utasitisha uhusiano nao.

Pindi watakapo hisi msimamo wako imara wataacha msimamo wao wa uchochezi na wewe na mke wako mtapata amani.

Lakini, bahati mbaya, baadhi ya mama na dada hawaachi tabia hiyo kwa urahisi na hukimbilia kwenye mashtaka yenye nia mbaya kama vile ugoni.

Tatizo linakuwa kubwa sana hivyo kwamba mwanaume anaweza akamtaliki au hata kumuua mke wake kwa sababu ya maneno ya mama yake.

Wanandoa vijana waliomba kutalikiana kwenye mahakama ya Tabriz. Mwanaume alisema mahakamani: “Mke wangu huandika barua za mapenzi kwa kaka yangu anayeishi Isfahan. Niliziona baadhi ya barua hizo chache jana usiku.” Mke wake alisema huku analia: “Mama mkwe wangu na wifi yangu hawanipendi na kunisumbua kila wakati. Lakini sasa kwa sababu matendo yao yenye fitina hayakumuathiri mume wangu, wameghushi barua kadhaa za mapenzi na wameziweka kwenye kabati langu la nguo ili wanichochee aniache.” Mahakama iliwasuluhisha wanandoa hao na kumshauri mume kumwambia mama na dada yake kuacha kufanyia vitendo viovu kwa bibi harusi wao.

Mwanamke mwenye umri wa miaka thelathini na nne alijimwagia mafuta ya taa na kujichoma moto. Majirani waliuzima moto haraka na walimpeleka hospitalini. Alipokuwa hospitalini mwanamke huyo alisema: “Mimi huishi na mume wangu na mama mkwe. Kila wakati huniona mimi nina makosa. Hutoa visingizio na kwa kawaida yeye ni mkali sana. Wakati wote haachi kusababisha ugomvi baina yangu na mume wangu. Jana nilikwenda madukani kununua vitu na ghafla nilikutana na rafiki yangu wa siku nyingi tulipokuwa tunasoma. Tulizungumza kwa muda mfupi halafu nilirudi nyumbani. Mama mkwe wangu alianza kuniuliza kwa nini nilichelewa? Nilimweleza lakini hakutosheka.

Aliniambia kwamba nilikuwa ninasema uongo na kwamba mwenye duka la nyama mtaani kwetu ni hawara yangu. Nilikasirika na kukata tamaa hivyo kwamba niliamua kujiua!”

Kwa hiyo, mwanaume kila mara anatakiwa kuwa na tahadhari na madai ya aina hiyo ambayo yanaweza kusababisha hatima ya hatari. Mume analazimika kufanya upelelezi kuhusu madai hayo kwa uvumilivu na asifanye uamuzi wa haraka.

Kama mambo yalivyo, wazazi wa mtu hufanya bidii na huteseka sana katika kumlea na kumkuza mtoto wao na hivyo huwafanya kuwa kituo cha matumaini yao yote. Wanamtegemea mtoto wao kuwa msaidizi wao watakapo kuwa wazee na mategemeo yao ni hayo tu. Kwa hiyo si haki mtu anapojitegemea asahau wajibu wake kwa wazazi wake. Lazima awatimizie matakwa ya hali zao hata baada ya kuoa.

Lazima adumise heshima yao na kuwa mnyenyekevu kwao. Anao wajibu wa kuwasaidia kwa kuwapa fedha endapo wanazihitaji. Si vema kusitisha uhusiano wake na wazazi wake na lazima awe anawaalika nyumbani kwake. Lazima amuamuru mke wake na watoto wake waoneshe heshima kwao. Lazima amwelekeze mke wake aelewe kwamba endapo atawaheshimu wazazi wake, hawataona, umuhimu wa kumuudhi na wanaweza hata kujivunia yeye na kumsaidia.

Mwisho, wanawake wanakumbushwa kwamba hawana haki ya kutarajia waume zao kuwaacha wazazi wao. Matarajio haya wala hayawezekani kuwa ya haki. Mwanamke mwenye busara anaweza kuwatembelea wazazi wa mume wake kwa namna ambavyo kwamba wanaweza kumchukulia yeye kama mwenzie muhimu katika familia yao. Hii inawezekana tu kama atawaheshimu, atataka ushauri kutoka kwao, akiwapa msaada na kadhalika.

Mazungumzo haya yameandikwa kwa kina kwenye sehemu ya kwanza ambapo unaweza kufanya rejea kwa taarifa zaidi.