Usipoteze Muda Wako Wa Akiba
Kazi za nyumbani huwa za aina nyingi mbali mbali. Kama mke anayo nia ya kufanya kazi kwa ubora zaidi hatoweza kuwa na muda wa kutosha wa kufanya kitu kingine. Huu ni ukweli hususan ambapo pia mama wa nyumbani anatakiwa kuwatunza watoto. Lakini wanawake walio wengi ambao wameolewa hupata muda wa akiba.
Kila mtu hutumia muda wake wa akiba kwa njia moja au nyingine. Wanawake wengine hupoteza muda wao wa akiba. Wanaweza tu kutembea mtaani au anazungumza na mwanamke mwingine. Mara nyingi mazungumzo yao ya saa chache hayana thamani yoyote. Wanaweza kusikiliza maneno ya kurudia rudia ambayo huthibitisha ni ya kupoteza muda na fadhaa.
Porojo za bure kama hizo husababisha kuvunjika heshima na maadili. Wanawake wanaopitia maisha ya namna hii, hakika wanapata hasara katika dunia hii na ile ijayo. Ni ajabu ilioje kwamba kama mtu yeyote anapoteza fedha, anatibuka sana, lakini watu hawafikirii hata kidogo kuhusu kupoteza muda wao wenye thamani katika maisha yao.
Mtu mwenye busara hujitahidi sana kutumia saa zenye thamani za maisha yake kwa manufaa. Ni mafanikio ya thamani kiasi gani mtu anaweza kuwa nayo!
Uvivu una madhara na husababisha maradhi ya akili na kuchanganyikiwa. Mtu mvivu wakati wote huwa katika mawazo na hutafuta njia za kuhisi huzuni.
Hupata aina nyingi za wasi wasi na baadaye akili yake huvurugika. Mtu mwenye furaha ni yule ambaye wakati wote anashughulika kufanya kitu fulani. Mtu mwenye bahati mbaya ni yule ambaye ni mvivu sana na hutumia muda wa ziada wa kutosha kufikiri raha na taabu za maisha yake. Kujishughulisha ni jambo la kufurahisha na uzembe ni chanzo cha mfadhaiko.
Je, si jambo la kusikitisha kwamba mtu anaweza kupoteza maisha yake yenye thamani au kutumia kiasi cha muda wake bila kunufaika kwa namna yoyote?
Bibi mpendwa! Unaweza kutumia kwa manufaa makubwa muda wako wa akiba. Unaweza kufanya kazi za kisayansi. Unaweza kununua vitabu vinavyo husiana na taaluma hiyo na kwa msaada wa mume wako, utaongeza ujuzi. Masomo ya kozi yoyote inawezekana, fizikia, kemia, Qur’ani, falsafa, historia, fasihi, saikolojia na kadhalika. Ungefurahia muda huo na labda siku moja ungetoa mchango wako kwa jamii kwa ujuzi wako. Unaweza kuandika makala au hata vitabu ambapo baadaye jina lako litaendelea kudumu. Pia unaweza kujipatia fedha.
Usidhani ya kwamba wanawake wote mashuhuri katika historia wanakuwa wakizembea. Wao pia waliolewa lakini ni hao ambao hawakupoteza bure muda wao wa akiba.
Bibi Dorothy Carnegie, alikuwa ameolewa na ambaye aliandika kitabu kizuri. Alikuwa akifanya kazi za nyumbani na pia alimsaidia mume wake (Dale Carnegie) kuandika kitabu chake maarufu; “How to make friends and Infuluence People.” Ameandika kwenye kitabu chake kuhusu kanuni za kumtunza mume: “Nimeandika kitabu hiki wakati mwanangu anapolala kwa muda wa saa mbili. Nilikuwa nasoma sana wakati ambapo nywele zangu zilikuwa zinakaushwa kwenye chumba cha kutengeneza nywele.”
Wapo wanawake wengi ambao wameandika vitabu maarufu wanapata mafanikio mengi katika uwanja wa sayansi.
Kama wewe ni mtu mwenye shauku, ungekuwa mmojawao. Kama mume wako ni mtafiti basi msaidie katika taaluma yake. Je, si jambo la kusikitisha kwa mwanamke msomi kutokutumia ujuzi wake wote?
Imamu Ali (a.s) alisema: “Hakuna hazina iliyo bora zaidi ya ujuzi.”
Imamu Baqir (a.s) alisema: “Yeyote anayetumia mchana na usiku kwa kutafuta ujuzi, kwa hakika ataunganishwa na neema za Mwenyzi Mungu.”
Kama wewe hupendelei kusoma au kutafiti basi jishughulishe na kazi za mkono au uchoraji kama kushona nguo, kupaka rangi, kufuma, mapambo ya maua, na kadhalika.
Unaweza kujifunza sanaa za aina hii na kuzifanyia mazoezi. Itikadi hizi zinaweza kukusaidia kiakili na kiuchumi. Uislamu pia umependekeza kazi za mikono zifanywe na wanawake wakati wa muda wao wa akiba. “Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: “Kusokota na kufuma ni burudani nzuri kwa wanawake.”