Hamu ya kuheshimiwa ni jambo la asili, lakini si kila mtu yupo tayari kuitoa. Mumeo hukutana na watu wengi katika shughuli zake wakati hayupo nyumbani. Baadhi ya watu hao wanaweza kuwa hawana staha na kumfedhehesha hali ambayo hatimaye humtibua mtu.
Wewe kama mke wake, anakutarajia wewe kuonesha heshima na ari akiwa nyumbani na kwa hali hiyo unaipandisha hadhi ya nafsi yake iliyokanyagwa.
Kumstahi na kumheshimu mume wako hakukudhalilishi wewe, lakini huongeza nguvu na mwelekeo kwenye harakati za kuyafanya maisha kuwa bora. Kila mara unatakiwa umsalimie na kwa hayo maamkizi yako mfanye ahisi unamjali. Usiingilie kati mazungumzo yake. Uwe na adabu na mpole unapozungumza naye na usimpigie makelele. Inapotokea wote wawili mnakwenda kwenye mkutano ngoja mumeo aingie kwanza. Msifie mbele ya watu wengine. Waambie watoto wenu kumheshimu baba yao na uwakaripie kama hawaoneshi adabu kwake. Mheshimu mbele ya wageni na uwe makini kwa mahitaji yake, na yale ya wageni.
Anapogonga mlango jaribu kufungua mlango huku ukitabasamu na kuonesha uso wenye furaha. Tendo hili dogo la kuonesha furaha, athari yake ni kwamba huburudisha moyo na kumwondolea uchovu mumeo. Baadhi ya wanawake wanaweza kudhani kwamba tabia ya aina hiyo si ya kawaida. Fikiria unapomwamkia mumeo kama mgeni. Hii si tabia nzuri kwa sababu mumeo amekuwa kwenye harakati siku nzima kwa ajili ya ustawi wa familia yake na anastahiki kufikiriwa na kuheshimiwa anaporudi nyumbani. Maamkuzi hayo ya kwanza huleta picha nzuri sana, na lililo zuri kwa mgeni ni zuri pia kwa jamaa wa familia.
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wajibu wa mwanamke ni kujibu hodi ya mlangoni na kumkaribisha mume wake.”
Imam Sadiq (a.s) alisema: “Mwanamke anayemheshimu mume wake na hamsumbui, atapata bahati na mafanikio.”
Mtukufu Mtume (s.a.w) alisema: “Mke anawajibika kutayarisha beseni na taulo ili mumewe anawe mikono.”
Uwe mwangalifu usije ukamfedhehesha mumeo, usizungumze naye kwa ukali, usimtukane, uwe msikivu kwake na usimuite kwa majina machafu. Ukimkosea na yeye atakufedhehesha wewe. Hatimaye, moyo wa mapenzi na kuaminiana utamomonyoka. Kwa hiyo, mtagombana mara kwa mara na kubishana, hali ambayo itasababisha mtalikiane.
Hata kama mtaendelea kuishi pamoja, maisha yenu kwa hakika yatajaa fujo. Hisia za uadui na usumbufu wa kisaikolojia unaweza kuanza kujengeka hadi kufikia kiwango cha kuhatarisha maisha ya wanandoa na hali hiyo inaweza kusababisha uhalifu. visa vifuatavyo vinaonesha baadhi ya mambo haya:
“Mtu mmoja mwenye umri wa miaka ishirini alimchoma kisu mkewe mwenye umri wa miaka kumi na tisa hadi akafa kwa sababu mke alimtukana mume. Mahakamani mume alisema; ‘nilimuoa mwanamke huyu mwaka moja uliopita. Mwanzoni mke wangu alinipenda sana. Lakini baada ya kipindi kifupi mke wangu alibadilika na kuanza kunidhalilisha.
Alianza kutumia lugha ya matusi kwangu kila ilipowezekana na kwa sababu ndogo sana, alianza kunikebehi. Kwa sababu jicho langu la kushoto ni kengeza, akawa na desturi ya kuniita mimi ‘punda kipofu.’ Siku moja, akaniita ‘punda kipofu’ nilikasirika sana hivyo kwamba nilimchoma kisu mara kumi na tano.’ ”
“Mtu mwenye umri wa miaka sabini na moja (71) ambaye alimuua mkewe, alitoa maelezo yafuatayo: ‘Ghafla tabia ilibadilika kwangu na akaanza kutonijali mimi. Wakati mmoja akaniita ‘mtu nisiyevumilika.’ nikagundua kwamba alikuwa hanipendi tena, nikamshuku na nilimuua kwa kumkata shoka mara mbili.”