Nyumba Nadhifu
Nyumba nadhifu hupendwa zaidi kuliko nyumba chafu katika njia nyingi:
Kwanza: unadhifu husaidia kuifanya nyumba ionekane safi, inavutia na mandhari ya kupendeza. Nyumba yenye mpangilio wa vitu, haimchoshi mtu, lakini itakuwa chanzo cha shangwe na furaha.
Mbili: kazi ya utunzaji wa nyumba ingekuwa rahisi kwenye familia inayofuata maagizo ipasavyo, na mama mwenye nyumba kwa kujua kwa usahihi mahali vilipo vitu vya nyumbani, haungepotezwa muda kuvitafuta. matokeo yake ni kwamba mwanamke hatachoshwa na kazi yake.
Tatu: humvutia mwanamume nyumbani kwake na mke wake. Nyumba yenye mpangilio mzuri ni mwakilishi wa sifa ya mwanamke.
Nne: nyumba nadhifu ni chanzo cha majivuno ya familia yote. Yeyote anayeitembelea, atapendezwa nayo, na kuvutiwa na ubunifu na ladha ya mwanamke.
Kuwa na vitu vya anasa si chanzo cha kuifanya nyumba kuwa nzuri, lakini ni jinsi ambavyo vitu vya ndani ya nyumba vilivyopangwa, huifanya nyumba iwe ya kuvutia. Lazima utakuwa umewaona watu matajiri ambao nyumba zao, licha ya kuwa na vitu vingi vya anasa, huchosha na wapo watu ambao ni masikini ambao nyumba zao, kwa sababu ya kuwa na mpangilio mzuri wa vitu, hufurahisha kuziangalia.
Kwa hiyo, kuipanga nyumba ni mojawapo ya wajibu wa mama wa nyumbani. Wanawake wenye vipaji na ladha nzuri wanajua namna ya kuziweka nyumba zao katika mpangilio mzuri, lakini kutaja mambo machache ni jambo linalofaa.
Ainisha vyombo vyako; usiviomekeze vyombo vyote pamoja. Weka vyombo vya kulia chakula yaani visu, vijiko, na kadhalika weka mahali pengine. Weka vyombo vinavyotumika wakati wageni wakiwepo, mahali tofauti na vyombo vinavyotumika kila siku. Fanya hivyo kwa kila kitu. Kila kitu lazima kiwekwe mahali pake hivyo kwamba watu wote wa familia wanaweza kuvipata kwa urahisi hata kwenye giza.
Baadhi ya wanawake wanaweza kuamini kwamba utaratibu wa namna hiyo ni kwa ajili ya watu matajiri. Lakini hii si sahihi hata watu masikini lazima wapange vyombo vyao pamoja na vyombo vya jikoni, vitanda, nguo na vitu vinginevyo.
Mathalani, mke lazima awe na mahali pa kuweka nguo zake tu na nguo za mume ziwekwe mahali pengine na nguo za watoto mahali pengine. Nguo za kuvaa wakati wa baridi lazima ziwekwe mahali tofauti na zile za kuvaa wakati wa joto. Nguo chafu lazima ziwekwe mahali pake. Mapambo kama vile; bangili, vidani, heleni, vibanio vya nywele na kadhalika lazima viwekwe sehemu yake. Wafundishe watoto wenu wawe nadhifu kuhusu nguo zao, vitabu vyao, wanasesere na kadhalika. Unaweza kuwa na uhakika kwamba kwa kuwa nadhifu, watoto wenu watajifunza na kuwaiga nyinyi wazazi wao.
Wanawake wachafu huwalaumu watoto wao kwa uchafu wa nyumba, ambapo watoto wanatakiwa kujifunza kutoka kwa wazazi wao.
Kama wazazi ni nadhifu, basi watoto watajifunza, na watoto kwa kawaida wapo tayari kukemewa kinidhamu.
Weka fedha yako yote, hati muhimu mapambo ya vito na vyeti mahali pa salama au mahali ambapo watoto hawafikii. Si sahihi kumwadhibu mtoto kwa sababu ya kugusa, kuharibu au kupoteza kitu chochote cha thamani ambavyo umeviweka mahali ambapo watoto wanaweza kufika. Wazazi ndio wenye hatia na wanatakiwa kutambua vema zaidi.
Mwanamume aliacha fedha na akamwambia mkewe aziweke mahali pa salama na akaziweka kwenye maungio ya shubaka na akaondoka.
Baada ya muda mfupi mwanamume akarudi na hakuzikuta fedha hizo alizoziacha. Aliangalia sehemu mbali mbali ndani ya nyumba kwa shauku lakini hakuzipata na akamuona mwanae wa umri wa miaka mitano alikuwa anachoma kitu bustanini. Mama wa mtoto huyo alimwendea kwa hasira, akamnyanyua juu, na halafu akamtupa mtoto huyo chini kwa nguvu sana hivyo kwamba mtoto huyo alikufa papo hapo. Mama aliogopa sana alipokuwa anaiangalia maiti ya mtoto wake. Mwanamke huyo alipotoka bustanini, mumewe alianza kumpiga na halafu akaamua aende polisi. Akapanda pikipiki yake lakini alipokuwa anaelekea polisi alipata ajali. Sasa yupo kwenye chumba cha wagonjwa mahututi!
Unadhani ni nani mwenye makosa kwenye tukio hili? Unaweza kuamua wewe mwenyewe. Lakini unajua tukio lingine linalofanana na hili.
Dawa, mafuta ya taa, petroli na vitu vingine vyenye asili ya sumu lazima viwekwe mahali ambapo watoto hawawezi kuvipata. Watoto hunywa na kula chochote kinachoonekana kama chakula au maji. Usihatarishe maisha yao kwa uzembe wako. Wapo watoto wengi ambao hufa kwa sababu ya uzembe wa wazazi wao.
Watoto wawili, kaka na dada, wenye umri wa miaka 6 na 4 walikunywa
D.D.T ya kuyeyushwa. Mtoto wa kike wa miaka minne alikufa na kaka yake alipona. Watoto hao walikuwa peke yao ndani ya nyumba. Walikunywa myeyuko huo kwa sababu ya kukata kiu. Mama yao watoto hao alisema hospitalini kwamba myeyuko huo ulitengenezwa kwa lengo la kuua panya ndani ya nyumba yake.”
Watoto wawili walikunywa mafuta ya taa kwa makosa wakidhani kwamba ni maji. Mtoto mwingine alimeza vidonge kumi miongoni mwa vidonge vya mama yake. Watoto hawa wote walipelekwa hospitalini kutibiwa.
Hatimaye unakumbushwa kwamba nidhamu inafaa tu hadi kiwango fulani ili isiwe sababu ya kukunyang’anya faraja. Usije ukashikwa sana na shauku kuhusu unadhifu, kwa sababu kuwa na shauku sana kwenyewe ni tatizo.
Mwanaume alisema: “Nimechoshwa na tabia ya mke wangu kushikilia usafi na unadhifu. Kila siku ninaporudi nyumbani saa 10:30 alasiri, mke wangu huniamuru ninawe mikono na miguu mara kadhaa. Anataka niweke nguo zangu mahali panapostahili. Haniruhusu nivute sigara kwenye vyumba vyote. Wakati wote nilikuwa naishi kwa uhuru, lakini wakati wa miaka minne ya ndoa, nimekuwa ninaishi jela. Kwa nini mtu ajali sana kuhusu usafi na unadhifu. Hii ni shauku iliyozidi mno, nami siipendi tabia hii.”
Tabia ya wastani ni bora sana katika vipengele vyote vya maisha ya mtu.
Mtu hatakiwi kuwa na vurumai sana hivyo kwamba inakuwa haiwezekani kuishi maisha ya kawaida, na pia si lazima mtu adekeze usafi hadi kwenye kiwango cha shauku iliyozidi mpaka.