Kuweza Kuishi Na Ndugu Wa Mumeo
Mojawapo ya matatizo ya kifamilia husababishwa na ndugu wa mume na mke wake.
Baadhi ya wanawake hawana uhusiano mzuri na mama wa mumewe, dada au kaka zake mumewe.
Kwa upande moja mke anaweza kujaribu kumtawala mume wake ili asiweze kumsikiliza hata mama yake au ndugu yake yeyote na anaweza kujaribu kuwafitinisha ili wasielewane wao kwa wao. Kwa upande mwingine, mama wa mume anajiona kuwa yeye ni mmiliki wa mwanae na mke wa mwanae.
Mama hujaribu sana kuwa karibu sana na mwanae na kutahadhari kwamba mke wa mwanae asiweze kummiliki mumewe kwa ukamilifu. Anaweza kusingizia uwongo kuhusu mke wa mwanae au kumuona anayo makosa.
Msimamo wa aina hii unaweza kufuatwa na mabishano mengi na hata chuki ya mara kwa mara. Hali inakuwa mbaya zaidi endapo watu hawa huishi kwenye nyumba moja. Hata kama ugomvi unaweza kutokea baina ya wanawake wawili, uchungu wa kiakili na dhiki hasa zaidi humpata mume aliyoko kati yao.
Mume ananaswa katikati ya mabishano ambapo hawezi kuegemea upande wowote. Kwa upande moja yupo mke wake ambaye angependa kuendesha maisha ya kujitegemea bila kuingiliwa na mtu yeyote. Kwa kawaida mume huhisi lazima amsaidie mke wake na amfurahishe. Lakini kwa upande mwingine, anafikiria wazazi wake ambao wamemsaidia kuingia katika maisha, wamemsomesha na wametumia muda mwingi wa maisha yao kumlea.
Anahisi kwamba wazazi wake wanatarajia awasaidie wakati wanahitaji msaada na kwamba haitakuwa busara kuwasahau. Zaidi ya hayo, kama yeye mwenyewe anayo haja ya kupata kitu fulani, hatakwenda kwingineko isipokuwa kwa wazazi wake, ambao watamsaidia yeye na familia yake. Matokeo yake ni kwamba anatambua kwamba marafiki zake wakuaminika ni wazazi wake na ndugu zake. Kwa hiyo, mtanziko kwa mtu mwenye busara ni ama kuwa upande wa mke na kuwaacha wazazi au kinyume chake, lakini hapana lolote kati ya haya mambo mawili yanawezekana.
Matokeo yake, atalazimika kwenda na pande zote mbili na kuziweza pande hizi katika hali ya kuridhika ambayo ni kazi ngumu. Njia moja tu inayoweza kurahisisha hali ni kwamba mwanamke lazima awe mwaminifu na mwenye hekima. Katika hali kama hii, mume anatarajia mkewe amsaidie katika kutatua tatizo.
Kama mke anamheshimu mama mkwe wake, humtaka ampe ushauri wake, na anakuwa mtiifu na kufanya urafiki naye basi, mama mkwe wake atakuwa msaidizi wake mkubwa sana.
Je, si jambo la kusikitisha kuona mtu ambaye anaweza kuwavutia watu wengi kwa sababu ya wema wake na tabia zake, halafu awafukuze kwa ajili ya ukaidi na ubinafsi wake? Hutambui kwamba katika mazuri na mabaya ya maisha, mtu anaweza akahitaji msada wa wengine, na hususan ule wa ndugu ambao wanaweza kukusaidia ambapo kila mtu akiwa amekukimbia? Je, si ni jambo zuri zaidi kufurahia uhusiano mzuri na ndugu wa mtu kwa kutumia busara na tabia njema? Je, hivi kweli ni busara na haki kufanya urafiki na watu wengine ambapo unavunja uhusiano na ndugu zako?
Uzoefu unaonesha kwamba mtu anapotaka msaada kutoka kwa wengine, marafiki humkimbia lakini ndugu aliwo watupa huja kumsaidia. Hii ni kwa sababu mshikamano wa kifamilia unao asili na hauwezi kuvunjika kwa urahisi. Kuna methali isemayo: “Hata kama nyama ya mtu ingeliwa na ndugu zake, wasingeitupa mifupa yake”
Imam Ali (a.s) alisema: “Mtu hawezi kamwe kuishi bila kuwa na ndugu zake, hata kama ni tayari na anao watoto.”
Mtu atataka heshima na wema wa ndugu zake. Ni wao ndio watakao msaidia kimwili na kiakili. Ni ndugu ndio wanasaidia mara nyingi. Wakati wa shida ndugu huweza kusaidia haraka zaidi kuliko wengine. Yeyote anaye watupa ndugu zake hupoteza mikono mingi, ya kumsaidia.
Mpendwa Bibi! Kwa ajili ya mume wako na faraja yako mwenyewe na pia kutafuta marafiki wengi na wanao kuunga mkono, vumilia kuwa nao ndugu wa mumeo. Usiwe mbinafsi na mjinga; uwe na busara na usisababishe usumbufu wowote kwa mumeo. Uwe mke mzuri na mwenye kujitolea ili uweze kukubalika kwa Mwenyezi Mungu na watu.