Kila mtu ana hamu ya urafiki na wema. Wote wanataka kupendwa na wengine. Moyo wa mwanadamu hunemeeka kwa hilo.
Mtu ambaye hapendwi na mtu yeyote anajifikiria yeye mwenyewe kama yupo peke yake na ametelekezwa. Bibi mpendwa! Mumeo hajawa tofauti. Yeye pia anahitaji mapenzi na huba. Kabla ya kuoa mapenzi na huba ya wazazi wake yalitimiza haja hii, lakini sasa, anayo matumaini kwamba wewe ndiye utakae timiza haja hii.
Mwanaume anategemea kwa mkewe kupata urafiki na mapenzi, ambyo ni haja ya wanadamu wote. Hujitahidi sana ili apate riziki na kukufurahisha wewe.
Hushirikiana na wewe matatizo yote ya maisha, na kama mwenza wako wa kweli, anajali kukufurahisha wewe kuliko hata wazazi wako wafanyavyo. Kwa hiyo, onesha shukurani zako kwake na umpende yeye, atakupenda wewe. Mapenzi ni uhusiano wa huku na huku ambao huunganisha nyoyo.
“Mvulana wa miaka ishirini ambaye alikuja Tehran kusoma kwenye chuo Kikuu, alimpenda mjane mwenye umri wa miaka thelathini na tisa ambaye alikuwa mama mwenye nyumba wake.” Hii ni kwa sababu mwanamke huyu aliijaza nafasi tupu iliyoachwa wazi na mama yake moyoni mwake kupitia wema wake.
Kama mapenzi yanatoka sehemu zote mbili, msingi wa ndoa unakuwa na nguvu na hatari za kutengana zinaepukwa. Usifikiri kwa majivuno kwamba mumeo alikupenda wewe alipokuona mara ya kwanza, kwa sababu mapenzi ya aina hiyo hayadumu. Mapenzi yanayodumu ni yale yanayopitia kwenye wema na huba ya kudumu katika namna ya urafiki wa karibu sana.
Kama unampenda mumeo na unao urafiki mzuri naye, atafurahi na atakuwa radhi kujitahidi na kujitolea kwa ajili ya ustawi wako.
Mwanaume anayefurahia mapenzi ya mkewe, husumbuliwa na maradhi mara chache au matatizo ya mshtuko. Kama mwamaume hapewi uhusiano mwema na wa kirafiki na mkewe anaweza kukata tamaa na kuanza kuikwepa nyumba yake. Anaweza kujikuta anatumia muda wake mwingi sana katika kutafuta marafiki na watu wa kumjali. Anaweza akajisemea mwenyewe: “Kwa nini nifanye kazi na kuwasaidia watu ambao hawanitaki. Inawezekana labda nikajifurahisha mwenyewe na kujaribu kupata marafiki wa kweli.”
Mwanamke anaweza akampenda mumewe kwa uaminifu, lakini mara nyingi haoneshi au kuyadhihirishi mapenzi yake.
Haitoshi kuanzisha uhusiano wa kirafiki na kuchukulia kwamba hali hiyo ni sawa. Matamshi ya mara kwa mara kama vile, ‘ninakupenda,’ ‘umepotea machoni kwangu sana,’ Ninafurahi kukuona,’ husaidia sana kuendeleza uhusiano mzuri. Mume anapokuwa safarini, mwanamke lazima amwandikie barua kuonesha kwamba haoni raha bila kumuona.
Kama ipo simu ofisini kwa mwanamume, mke anatakiwa kumpigia simu mara kwa mara, lakini isizidi kiasi. Mke amsifu mumewe kwa marafiki na ndugu zake wakati hayupo, na kumtetea endapo mtu anamsema kwa ubaya.
Mwenyezi Mungu Mweza wa yote anazungumzia kuhusu mapatano haya ya mapenzi na huba ya mume na mke ndani ya Qur’an:
وَمِنْ آیَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَکُمْ مِنْ أَنْفُسِکُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْکُنُوا إِلَیْهَا وَجَعَلَ بَیْنَکُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِی ذَٰلِکَ لَآیَاتٍ لِقَوْمٍ یَتَفَکَّرُونَ
“Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wenza kwa ajili yenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. hakika katika haya bila shaka; zipo Ishara kwa watu wanao fikiri ”.(Quran 30:21)
Imam Ridha (a.s) alisema: “Wanawake wengine ni baraka kwa waume zao ambao huonesha mapenzi na huba yao.”
Mtukufu Mtume (s.a.w.w) alisema: “Watu walio bora sana miongoni mwa wanawake ni wale wenye mapenzi na huba.” Imam Sadiq (a.s) alisema: “Ukimpenda mtu mwoneshe kwamba unampenda.”