پایگاه اطلاع رسانی آیت الله ابراهیم امینی قدس سره

Saidia Kufanya Kazi Za Nyumbani

Saidia Kufanya Kazi Za Nyumbani

Licha ya kwamba utunzaji wa nyumba ni wajibu wa wanawake, lazima ieleweke kwamba kuendesha mambo ya nyumbani si kazi rahisi.

Mke ambaye ni mama wa nyumbani hata akitumia muda kiasi chochote kile kwa utunzaji wa nyumba, hatoweza kumaliza kazi hiyo yote kwa wakati moja. Hii ni kweli hasa zaidi pale ambapo anatakiwa kuwakirimu wageni au anapougua na kadhalika. Kazi ya kutunza nyumba humchosha mke wa nyumbani na hivyo wanaume wanatarajiwa kuwasaidia wake zao katika suala hili.

Si haki kwamba mwanamume awe amekaa nyumbani bila ya shughuli yoyote ambapo mke wake anashughulika na kazi nyingi mbali mbali. Inafaa tu mume kumsaidia mke wake kadiri iwezekanavyo na wakati wowote awezapo. Msaada huu ni ishara ya huba ambayo humvutia mke kwa mume wake na familia yake.

Si ujasiri wa kiume hata kidogo kwamba mwanaume hapaswi kugusa kitu chochote ndani ya nyumba, bali kutoa amri tu kumpa mkewe. Nyumba ya familia si makao makuu ya kutoa amri, isipokuwa hapo ni mahali pa upendo, wema na ushirikiano.

Bwana mpendwa! Usidhani kwamba wewe ukifanya kazi za nyumbani ni kushusha hadhi yako. Kinyume chake ni kwamba, mke wako atapendezwa sana na kitendo chake cha kumsaidia.

Mtume (s.a.w.w) wa Uislamu ambaye ni mtu anaye heshimiwa sana katika historia, alikuwa na desturi ya kusaidia kazi za nyumbani.

Ayisha, mke wa Mtume (s.a.w.w) alisema: “Wakati wowote Mtume

(s.a.w.w) anapokuwa hana kazi, alikuwa na desturi ya kushona nguo zake, kutengeneza viatu vyake na alikuwa anafanya kazi nyumbani kama wanaume wengine.”