Mwanamke Asiye Mwaminifu
Mara tu mwanamke akionekana ana hatia ya kuzini, kwa kutumia uthibitisho madhubuti, mume wake atakuwa katika hali ngumu sana. Kwa upande moja heshima yake inakuwa hatarini na kwa upande mwingine kuvumilia fedheha ya aina hii si rahisi.
Anahisi amenasa kwenye mtego wa kutokuafikiana ambamo si rahisi kujinasua.
Mwanamume aliyeko kwenye hali hii anaweza kuchagua kufanya mojawapo ya haya yafuatayo:
(a) Anaweza kunyamaza kimya kuhusu jambo lenyewe ili aokoe heshima yake na kwa ajili ya familia yake.
Lakini lazima ataishi akikumbuka jambo hili katika maisha yake yote. Kama mambo yalivyo chaguo hili halikubaliki kwa mtu yeyote mwenye kuheshimika, kwani haitakuwa rahisi kuvumilia kuishi na mke wake mzinzi na uwezekano wa kupata mtoto wa haramu. Mapenzi makali ni sifa inayopendeza sana kwa mwanamume hivyo kwamba mwanamume ambaye hana sifa hiyo hawezi kufurahia neema ya Mwenyezi Mungu Mweza. Ni maisha ya fedheha na aibu ilioje watu hao walio nayo ambao hawajali kutokuaminika kwa wake zao. “Mtume (s.a.w.w) alisema: ‘Harufu nzuri ya Peponi yaweza kunuswa katika umbali wa safari ya miaka mia tano, lakini makundi mawili ya watu yatanyimwa; nayo ni wale watu ambao wamelaaniwa na wazazi wao na mume wa mke aliye zini.’ Swali liliulizwa; ‘Ewe Mtume (s.a.w.w) wa Mwenyezi Mungu; nani huyu mume wa mke aliyezini? Mtume alijibu: ‘Mwanaume ambaye anamjua mke wake kuwa ni mzinzi, na hunyamaza kimya kuhusu suala hili.’ ”
(b) Angeweza kumuua mwanaume aliyezini na mke wake au wote wawili mke wake na mwanaume mzinifu. Anaweza kulipa kisasi na kupata amani. lakini tendo hili ni la hatari kwani halingekuwa na mwisho mzuri, kwa sababu mauaji hayangefichwa daima milele. Muuaji lazima angejulikana na kuadhibiwa. Hangeweza kuthibitisha kutokuaminika kwa mke wake ndani ya mahakama; na kwa hiyo uwezekano wake kuachiliwa kutoka jela ungekuwa mdogo sana. Ingewezekana hata kupewa adhabu ya kifo. Hivyo angepoteza maisha yake na watoto wake wangekengeuka. Kwa hiyo, si busara kwa mwanaume kuhatarisha maisha yake kwa sababu ya kulipa kisasi. Mwanaume anatakiwa kuwa na busara na mtaratibu na kuweza kudhibiti hasira yake hadi apate ufumbuzi unaofaa kwa tatizo lake.
Angejiua ili asiendelee kuona kutokuaminika kwa mke wake na aishi maisha ya fedheha. Tendo la kujiua wala si lenye busara kwa sababu upande moja amejiua, ambayo yenyewe ni dhambi kubwa katika Uislamu na muuaji lazima aadhibiwe na Mwenyezi Mungu mnamo Siku ya Hukumu. Kwa upande mwingine amejinyima maisha. Hii ni mantiki ya aina gani ambayo ingeshawishi kujiua kama kisasi cha uhalifu wa mtu mwingine.
Angeteseka katika maisha yajayo na pia kumpa uhuru mkubwa zaidi mke wake kuendelea kuzini zaidi.
Angemtaliki mke wake. Hiki ni kitu cha busara zaidi kufanya. Ni sahihi kwamba talaka ingeharibu maisha ya familia yake na ingeleta madhara zaidi kwake na watoto wake, lakini hakuna njia nyingine yeyote. Ni bora zaidi yeye kumtaliki mke wake na achukue watoto wake, kwa sababu si sawa kuwaacha waishi na mama yao mwovu.
Kama mambo yalivyo, kulea watoto si kazi rahisi kwa mwanaume, lakini lazima ahakikishe kwamba Mwenyezi Mungu angemsaidia. Angemsaidia yeye kuendesha tabia ya kuheshimika.